Thursday, October 12

Vijana kusakwa Songwe kwa kutelekeza wazazi


Mbozi. Mkuu wa Mkoa wa Songwe,  Chiku Galawa ameagiza viongozi wa serikali za vijiji na kata kuwakamata vijana wote wanaokimbilia mijini na kuacha  kuwahudumia wazazi wao ili washughulikiwe kwa kosa la kuwatelekeza.
Amesema lazima serikali za vijiji na kata zichukue hatua kwa vijana wa aina hiyo kwani wanafahamika ili kuwalazimisha kutimiza wajibu wao wa msingi wa kulea familia zao lakini pia kulea wazee wao ambao walitumia nguvu nyingi kuwalea  wao wakiwa vijana.
Kauli hiyo ameitoa leo Alhamisi akiwa Kijiji cha Zelezeta wilayani Mbozi mkoani hapa alipotembelea wanufaika wa mradi wa mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).
“Naagiza hawa vijana wanafahamika hivyo lazima watafutwe, wakamatwe na wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria,’’ amesema na kuongeza kwamba
“Hakuna mwenye hati miliki ya ujana kila mmoja ni mzee mtarajiwa, kama ukishindwa kulea wazazi wako leo wanao wanakuona nawe hawatakulea utakapokuwa mzee hivyo kuweni na upendo waleeni wazee, pia vijana acheni tabia ya kuzaa bila mpango na kuwatelekeza watoto wenu tumieni rasilimali ardhi mliyonayo kujipatia kipato,” amesema Galawa.
Mbali na hilo, Galawa ametoa mwezi mmoja kuanzia leo Alhamisi kwa halmashauri zote mkoani hapa kuwalipia bima ya afya (CHF) wazee wote ili waweze kutibiwa wanapohitaji huduma hiyo.
Mmoja wa wanufaika wa mpango wa Tasaf,  Elina Mwandaghasya (89) Mkazi wa Kijiji cha Zelezeta akizungumza kwa shida kutokana na uzee, amesema ana watoto saba ambapo mmoja ni mstaafu wa jeshi lakini amekuwa mlevi wa kupindukia na wengine wanaishi nje ya kijiji hicho na wana uwezo mzuri kiuchumi lakini hawamkumbuki kwa chochote kile.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Zelezeta,  Japhet Buya amesema kijiji kilimwingiza kikongwe huyo katika mpango wa Tasaf ili kunusuru hali yake kutokana na watoto wake kutomjali na wengine kukimbilia mjini na kumwacha akiwa hana makazi bora ya kuishi na kuamua kumjengea nyumba kwa fedha za mpango.
Buya  amesema awali mzee  huyo alikuwa akichukuliwa fedha za mfuko huo  na mmoja wa watoto wake lakini baada ya kufuatilia ilibainika alikuwa akitafuna  na kufanyia matanuzi binafsi fedha hizo.
Amesema, “Tulipogundua hilo Serikali ya kijiji iliingilia kati kuzuia fedha hizo kisha kuanza kuziwekea mazingira mazuri kupitia Serikali yake kwa kumjengea nyumba ambapo wananchi walichangia tofali huku kanisa la Moravian na kijiji wakinunua bati.”

No comments:

Post a Comment