Hali ya taharuki imewakumba wananchi wa mji mdogo wa Mbalizi leo Jumatano baada ya mtu au watu wasiojulikana kuvumishwa kuwa mwanamke huyo baada ya kushindwa kutua tenga alikimbilia kituo cha Polisi Mbalizi kuomba msaada.
Uvumi huo ulieleza kuwa, mwanamke huyo aliimba nyanya sokoni Mbalizi.
Katika tukio hilo jana mchana Polisi walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliovamia kituo hicho ili kumuona mtuhumiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga amesema uvumi huo ulienezwa na watu au mtu asiyejulikana kwamba kuna mwanamke aliiba tenga la nyanya sokoni Mbalizi lakini alipojaribu kulishusha kutoka kichwani ilishindikana, hivyo akaamua kwenda kituo cha polisi kuomba msaada.
“Wakati wa taharuki kama ile kila mtu anakuwa na tabia na nia yake, ndiyo maana imelazimika kutumia nguvu kidogo kuwanyamazisha watu kwa mabomu. Ule ni uvumi tu ambao hata hatujamfahamu aliyeeneza alikuwa na mlengo gani kwa kuwa hakuna tukio kama hilo,” amesema.
Kamanda Mpinga amesema sasa hali ni shwari na wananchi wameelimishwa wakaondoka kwenda sehemu zao za biashara na shughuli nyingine.
Mwenyekiti wa Soko la Mbalizi A ambako kituo cha polisi kipo, Geofrey Msigwa amesema hakuna kitu kama hicho bali naye aliona watu wengi wakielekea kituoni jambo lililosababisha polisi kuwatawanya kwa mabomu.
Amesema, “Hii ni hatari kwa mtu kusikia jambo bila kulifanyia utafiti na kuanza kulizusha bila kutambua athari inayoweza kutokea.”
Amelaani kitendo hicho akisema kinahatarisha usalama na amani.
Pia, amewaonya watu kutokimbilia vitu ambavyo ni vya kusikia bila kuvifanyia uchunguzi kwa kuwa inaweza kuwagharimu.
Msigwa amesema hawana taarifa za wizi huo na wanashangazwa na uvumi huo.
No comments:
Post a Comment