Dk Ndugulile alisema lengo ni kuhakikisha mashirika hayo yanafanya kazi kulingana na uanzishwaji wake.
Aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana alipozungumza na watumishi wa Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, kujitambulisha kufuatia kuteuliwa hivi karibuni na Rais John Magufuli.
Alisema licha ya idara hiyo kuwa na kanzi data kwa ajili ya NGO, lazima ifuatilie utendaji wa mashirika hayo kwa kuwa baadhi yake yamekuwa yakienda kinyume na malengo.
“Ni vizuri NGO za kimataifa ziwe na sura ya kimataifa na zile za kitaifa zibaki na sura hiyo, wakati mwingine hasa kipindi cha uchaguzi baadhi ya mashirika hayo hujishughulisha na siasa na kuacha malengo yake,” alisema.
Kuhusu huduma za jamii kwa wazee, Dk Ndugulile alisema licha ya jitihada zinazofanywa, eneo hilo lina changamoto kubwa hususan katika misamaha ya huduma za afya na nyumba za kuwahifadhia.
Dk Ndugulile alisema wakati mwingine vituo vya kuhifadhia wazee vimelazimika kufungwa, au kusaidiwa na watu wengine tofauti na idara husika.
Naye Msajili wa NGO, Marcel Katemba alimweleza Dk Ndugulile kuwa idara hiyo inaendelea na uhakiki wa mashirika yasiyo ya Serikali nchini, lengo likiwa ni kuhuisha orodha na kuboresha kanzi data ili kupima utekelezaji wa majukumu yake.
Katemba alisema Tanzania ina mashirika yasiyo ya Serikali yapatayo 9,000 na kwamba, uhakiki huo utaisaidia idara hiyo kufuatilia shughuli za NGO kwa ukaribu.
No comments:
Post a Comment