Sunday, October 22

Ustaa ni sehemu ya dawa za kulevya


Ustaa wa Kibongo unakulazimisha kutanua mikono. Kuinua mabega. Kuvimba kifua. Kutembea kijivuni. Kutumia simu tatu tatu. Na zaidi wa kiume kumiliki totoz za kutosha na staa wa kike kumilikiwa na idadi kadhaa ya madanga. Iko hivyo.
Msichana mwenye umaarufu Kibongobongo, hata kama alilelewa kwenye mazingira ya Kiparokia au Kimadrassa. Akishapata jina hugeuka kama kinyonga. Wengi wao wanabadili gia angani kama Chadema na Dr Slaa 2015.
Ama kwa kutaka wenyewe au kwa kulazimishwa na mazingira. Leo ukitaka kumtengeneza staa wa kike Bongo kwenye sanaa yoyote itakupa wakati mgumu sana.
Mifano hai ipo mingi sana. Mzazi kukupa mwanaye umtengeneze kimuziki au kifilamu, inabidi umpate mzazi mwelewa.
Lakini hawa wa kubebeana mabwana na kujitapa mitandaoni kuwa kama mfano kwa Mzee wa Kichaga akupe Binti yake Manka eti unataka kumkuza kisanii. Thubutu.
Mazingira haya ya kudhani kuwa umaarufu ni daraja la kujivisha Ufalme Mswati, kwa miaka mingi tumeendelea kutengeneza masikini wenye majina makubwa.
Nitakushangaa ukishangaa kwa nini wazee wetu waliovuma miaka hiyo wameishia kuzikwa bila kitu.
Msanii wa Kitanzania anapokuwa yupo juu kwenye kilele cha umaarufu na umiliki wa bomba la kuingizia pesa hujisahau.
Ustaa wa Kibongo una maradhi fulani kichwani yanayofanya vijana wenye umaarufu waamini kuwa wameumbwa kwa ajili ya bata.
Hawajaumbwa kuja duniani kuwekeza maisha bali pesa kuwekeza kwenye miili yao.
Wengi wameshituka kukiwa kumekucha. ‘Stress’ zinawachanganya. Wanatamani muda urudi nyuma kitu ambacho hakiwezekani.
Muda hauna urafiki na maisha ya binadamu. Muda ndo talaka pekee ambayo hata msela, muhuni, paroko au shekhe ajutie. Talaka ya muda haichagui mtu. Ukiyatenda tofauti maisha yako kwenye muda muafaka huna ujanja mwingine zaidi ya shingo kuelekea kibra na kusubiri majuto.
Wakati wa kutengeneza pesa, walitengeneza nyingi sana. Wakaziacha zielee hewani bila mizizi. Hawakutaka kuwekeza kwa baadaye.
Na wengine hata akaunti walikuwa hawana. Ziliingilia mkono wa kulia na kutoka mkono wa kushoto. Mifuko ya mashati na suruali na mikoba ikawa ndiyo akaunti zao. Vicoba vyao. Uwekezaji wao.
Hawakutaka kusumbuka mambo ya kusaini saini juu ya meza pana kwenye mabenki yetu. Wapo waliobadili ngozi zao kutoka kwenye rangi za antena mpaka rangi za ving’amuzi.
Wapo wale walioona haitoshi wakatengeneza tattoo kwa pesa nyingi kwenye ngozi zao laini. Muda hauna ushikaji. Leo hii wanaamka jua likizama. Wajanja waliwatumia. Wao wakashindwa kutumia majina yao kuzifanya pesa ziwe nyingi halafu zidumu. Kuna pesa na pesa nyingi.
Katika ubora wake ilikuwa ngumu kuwaza ubunge wa viti maalumu. Katika wakati wake akiwa anavutia kwa jina lake, ngozi, meno na macho, ilikuwa ngumu sana kuwaza kuandaa kitu siku ya Valentine ili apate pesa.
Alipofanya vyote hivyo hapa mwishoni. Taa nyekundu ziliwaka kwenye vichwa vya watu timamu. Kuwa muda umewadia ule wa kutamani urudi nyuma na kuanza upya.
Bila kuandaa au kujiingiza huko. Bado
pesa angepata huku akikwepa usumbufu wa simu za kila mwenye pesa ambaye angetamani kubarikiwa kwa kuupapasa mwili wake.
Kifupi ni kwamba haikuwa na maana mtu kumiliki pesa nyingi halafu ukashindwa kujihifadhi kwenye mbavu laini za kiumbe huyu. Pesa yako itakuwa ‘inanuka’ haina thamani.
Pesa ya Tanzania matumizi yake huenda sambamba na utajiri wa kumiliki viumbe sahihi kwa matamanio ya macho na roho uzao wa Eva.
Aliitawala Tanzania. Akaiteka mashariki ya Congo. Akifika Leaders Club pale hata nyasi na ile miti isiyo na afya vilimtii.
Uwanja na wadudu waliopo ndani yake vingemnyenyekea kwa kuruhusu nyayo zake laini zipite.
Akaiweka kwapani Rwanda nzima na Kagame wao. Wakati kuna wanawake wenzake wanapata misukosuko kwa kutamani tu kufika Ikulu ya Rwanda, yeye aliombwa na Ikulu yenyewe afike kutia baraka.
Kuna wakati mtu anakuwa juu kiumaarufu mpaka haielezeki. Ndivyo alivyokuwa huyu. Mrwanda mmoja akaamua kuweka ndani kabisa. Hakusikiliza la muadhini wala mnadi swala.
Kwa wakati ule hata leo hii bado ni sehemu ya binadamu uzao wa Eva wenye mvuto. Ukimuona atakuvutia. Mlemavu wa macho tu ndo anaweza kushindwa kuvutiwa naye. Ni mwenye uzuri uliokamilika. Mtoto mzuri halafu kakulia mjini.
Irene Uwoya. Leo hii anafanya biashara ambayo angeifanya miaka kadhaa nyuma wakati huo Wadosi pale Kariakoo wanatetemeka wakimuona. Leo angekuwa miongoni mwa wasichana matajiri mjinii.
Katika utawala wa JK. Na yeye akitembea kwenye ncha ya kilele cha mlima wa umaarufu. Angepiga pesa nyingi sana.
Pamoja na kwamba mtaani hali ni ngumu. Bar nyingi mjini zinawahudumu wengi kuliko wateja. Lakini bado neno “Kwa Irene Uwoya’ lipo sana kwenye vinywa vya watanua makoo kwa mtungi.
Uwoya hataki tena ujinga anamiliki bar mitaa ya Sinza Mori.
Tatizo pesa ambazo zingemfanya awe mfanyabiashara mkubwa sana kwa aina yaa biashara yenyewe, nyingi ziko jela.
Nyingi ziko mahabusu. Nyingi zinajificha au kukimbia nchi.
Waliokuwa maarufu kwa jina la Mapedeshee wametoweka. Ndo maana hata bendi za dansi zinapumulia gesi ICU. Hakuna pesa za mchezo mchezo mtaani. Kuna vitu Magufuli kafanya lazima utafakari. Achana na Bunge Live hata wabunge wa CCM wanatamani kuuza sura. Ila ule upuuzi wa kumuogopa mtu haupo. Sijui mpuuzi tu kumtishia askari barabarani haupo. Mambo ya unanijua mimi nani? Imebaki historia.
Pedeshee mmoja alikuwa na uwezo wa kuingia bar na wasichana wake kibao na wapambe juu wa kuipamba meza yake.
Angefunga kaunta ya Bar ya Uwoya. Shughuli ingeishia hapo. Ingekuwa inafanywa hivyo kila siku au kila mwisho wa wiki. Mapedeshee wangeweka himaya katika bara yake.
Hao ndiyo waliokuwa wanaleta pesa za masihara kwenye biashara kama hizo. Hawapo siku hizi. Pale Leader’s Club mastaa wa kike walikuwa wanakusanywa kuosha magari. Pedeshee mmoja angeleta gari lake na kutaka kuoshewa na staa flan wa kike kwa laki tano.
Manaake ni kwamba kama pedeshee mmoja alioshewa na Uwoya gari moja kwa milioni. Kwa sababu ya uwepo wa Uwoya tu. Hii leo angefanya nini kwenye Bar ambayo Uwoya ndiye mmiliki?
Mapedeshee wangetawanya pesa sana ili kuhudumiwa na Uwoya. Angepiga pesa. Pesa nyingi.
Lakini wakati ule mastaa nao walitaka kuishi kipedeshee. Ilikuwa rahisi kusikia Irene Uwoya kamtuza laki tano Kalala Junior jukwaani.
Wakaishi kipedeshee badala kutumia fursa hiyo kutengeneza mazingira ya pesa nyingi. Ndivyo ilivyo hata kwa mastaa wa kiume.
Walioshuka kisanii na kimapato ni kwa sababu ya kutojua chochote cha upande mwingine. Wakakariri kuwa kila siku wataishi kwa pesa za shoo na mauzo ya albamu.
Hapo ndipo utaona tofauri kubwa sana ya Lady Jaydee na wanamuziki wenzake wa kike. Na ndipo utamtofautisha Dk Cheni na waigizaji wengine. Walijua kuandaa mazingira ya nje ya boksi la filamu na muziki.
Ukiangalia maisha ya mastaa wengi ambao walisahau kuwekeza pesa nje ya mfumo wao. Ni rahisi kusema kuwa Ustaa wa Bongo ni sehemu ya dawa za kulevya.
Madhara ya ustaa wa Bongo ni yale yale. Wengi wamefeli kwa njia moja tu kama ilivyo watumiaji wa dawa za kulevya.
Waliojisahau leo wanawekeza biashara ambazo walitakiwa kuwa nazo miaka mingi nyuma na kutengeneza pesa za kutosha mapema.
Tofauti na leo mbali ya kutoweka kwa mapedeshee pia masharti ni mengi kama kufungua jioni na kufunga masaa kadhaa baada ya jioni.

No comments:

Post a Comment