Tuesday, October 3

Ushahidi kesi ya vigogo Tanesco Novemba 2




Dar es Salaam. Usikilizaji wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili watumishi watano wa zamani wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na msambazaji kutoka kampuni ya M/S Young Dong Electronic Co. Ltd utaanza Novemba 2 na 3 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) washtakiwa wanadaiwa kuisababisha Serikali hasara ya Sh275 milioni.
Washtakiwa hao ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Robert Shemhilu; Ofisa Ugavi, Harun Mattambo; Mkurugenzi wa Fedha, Lusekelo Kasanga; mwanasheria, Godson Makia na msambazaji, Martin Simba.
Usikilizaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka unatarajiwa kuanza Novemba 2 na 3 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka mawili ya uhujumu uchumi na matumizi mabaya ya madaraka, hivyo kusababisha hasara ya Sh275 milioni.
Upande wa mashtaka unawakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Vitalis Peter.
Wanadaiwa kati ya Januari na 
Desemba 2011 katika ofisi za Tanesco, Ubungo washtakiwa wakiwa waajiriwa wa shirika hilo walitumia madaraka yao vibaya kufanikisha malipo kwa msambazaji Martin Simba bila kufanya uhakiki.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo kinyume cha kifungu cha 35 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma namba 21 ya 2014 kitendo ambacho kilisababisha msambazaji huyo kupata faida.
Inadaiwa kati ya Januari na Desemba, mwaka 2011 katika ofisi za Tanesco, Ubungo washtakiwa wakiwa waajiriwa wa shirika hilo pamoja na msambazaji huyo waliisababishia Serikali hasara ya Sh275 milioni. Washtakiwa wapo nje kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment