Tuesday, October 3

MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Namna bora ya kujibu maswali ya kifasihi


Baadhi ya wasomaji waliojitambulisha kuwa ni watahiniwa tarajali wa mtihani wa kidato cha nne mwaka huu, wameiomba Mbalamwezi ya Kiswahili iwaelekeze namna bora ya kujibu maswali hususan ya fasihi andishi katika mtihani wa Kiswahili. Suala hili ni muhimu kwa kuwa mtahiniwa anaweza kuwa na hoja nzuri lakini akafeli kutokana na uratibu na uwasilishaji wake mbaya.
Katika ufafanuzi wetu, tutatumia swali hili kama mfano: “Kwa kutumia vitabu viwili vya riwaya ulivyosoma, jadili umuhimu wa mandhari katika riwaya.”
Kabla ya kujibu swali, mtahiniwa hana budi kulisoma swali hilo kwa makini na kujiridhisha kuhusu mahitaji ya swali hilo. Baada ya kupata uhakika wa kile anachotakiwa kujibu, mtahiniwa atapaswa kujibu kwa kuzingatia sehemu kuu tatu yaani utangulizi, kiini cha swali na hitimisho. Ikumbukwe kuwa kila kipengele kina alama zake. Mtahiniwa akiacha kuzingatia kipengele kimoja wapo atakuwa amepoteza alama za kipengele hicho.
Katika utangulizi, mtahiniwa anapaswa kutoa ufafanuzi wa dhana za msingi na kutaja vitabu atakavyovitumia kujibia swali hilo. Kwa kurejelea swali letu la mfano; mtahiniwa atatakiwa kueleza maana ya mandhari katika kazi ya kifasihi. Aidha, aeleze kuwa kila mandhari hutumiwa kwa makusudi maalumu. Baada ya kufanya hivyo, ataje riwaya mbili atakazotumia kujibia swali hilo na waandishi wake.
Katika sehemu ya kiini cha swali; mtahiniwa aanze na kitabu kimoja wapo kutoa hoja na kuzifafanua. Mtahiniwa hana budi kufanya marejeo katika riwaya husika kila mara katika maelezo yake. Atafanya hivyo kwa kitabu cha kwanza kisha kwa kitabu cha pili. Hapaswi kutoa historia ya kitabu au kusimulia kisa kizima bali ajibu tu kile kinachohitajika. Mathalani, hoja moja wapo inaweza kuwa, ‘Mandhari ya dampo inaibua dhamira ya umaskini’ kisha atoe ufafanuzi.
Ni vema kila hoja iandikwe kwa mtindo wa sentensi na ieleweke bayana. Aidha kila hoja iwe katika aya yake yenye walau mistari sita hadi minane. Mtahiniwa akimaliza kitabu cha kwanza aingie kitabu cha pili.
Idadi ya hoja kwa kila kitabu hutegemea na swali. Kama idadi ya hoja imetajwa, mtahiniwa azingatie hilo. Ikiwa idadi ya hoja haikutajwa, mtahiniwa aandike walau hoja nne kwa kila kitabu. Ikumbukwe kuwa, kiini cha swali ni sehemu yenye alama nyingi zaidi. Hivyo, hoja ziwe bayana, maelezo kuntu yatolewe yakishadidiwa na mifano dhahiri kutoka vitabuni. Wakati mwingine ikiwa swali ni la kulinganisha au kulichanganua dhamira au masuala mengine kutoka vitabuni, basi mtahiniwa hana budi kuandika kwa kuhusisha mawazo hayo. Kwa sababu hiyo, kila hoja itabeba maelezo kutoka katika vitabu vyote viwili.
Kipengele cha mwisho ni hitimisho. Sehemu hii ndiyo inayofunga mjadala wa majibu ya swali zima. Watahiniwa wengi hawajui kutoa mahitimisho. Inawezekana ni kosa lao, lakini pengine hawajapewa mazoezi ya kutosha kuhusu kuhitimisha mjadala. Hitimisho hutegemea na aina ya swali; mtahiniwa atatakiwa kueleza kwa muhtasari, kushadidia hoja zake, kuibua changamoto, n.k. kwa kuzingatia swali lilivyo. Haitoshi tu kuhitimisha kwa kusema, ‘Huu ndio umuhimu wa mandhari katika vitabu hivi.’ Hitimisho litolewe katika walau katika mistari sita.
Masuala mengine ya kuzingatiwa ni kwamba, mara zote jina la kitabu linapotajwa halina budi kupigiwa mstari. Majina ya mashairi yanapotajwa hayana budi kuwekewa alama za mtajo mathalani, “Asali Lipotoja”. Aidha, unukuzi wa beti za mashairi na majibizano ya wahusika katika tamthiliya, haviwekewi alama za mtajo.

No comments:

Post a Comment