Rais wa Marekani Donald Trump Jumatano aliwaahidi wamarekani watakuwa na fedha nyingi za kutumia kama wabunge wanaidhinisha mpango wake wa mageuzi ya kodi.
Rais Trump akiwa katika uwanja wa ndege huko Harrisburg kwenye jimbo la Pennsylvania aliwambia madereva wa malori kwamba familia ya kawaida ya kimarekani itapata nyongeza ya mshahara ya dola 4,000 kutokana na mabadiliko anayoyataka japokuwa wachumi wanasema mafao hayo yataonekana katika kipindi cha zaidi ya miaka minane kwa kiwango cha kiasi cha dola 500 kila mwaka.
Hotuba ya Rais Trump kwa mamia wa madereva wa malori ambayo ni ajira ya kawaida katika majimbo 50 ya nchini Marekani ilipangwa kupinga maoni ya wachambuzi huru wanaoeleza kwamba mabadiliko hayo ya chama cha Republican yatawasaidia zaidi wale wenye mapato ya juu.
Hotuba ya rais huko Pennsylvania haikueleza kwa kina juu ya namna mpango wake utakavyowafaidisha matajiri. Alisema marafiki zake matajiri wamemwambia hawataki kitu chochote kutoka kwenye pendekezo lake na wanamuomba kuwapatia watu wa daraja la kati.
No comments:
Post a Comment