Monday, October 23

TANZANITE ONE: TUPO TAYARI KUPITIA MKATABA UPYA

 


KAMPUNI ya TanzaniteOne  imesema ipo tayari kujadiliana na Serikali   kupitia upya mkataba wake na kufanya mapitio ya taratibu zote za uchimbaji na biashara ya madini hayo.
Msimamo wa TanzaniteOne  ulitolewa   jana na Katibu wa Kampuni hiyo, Kisaka Mnzava.
Alisema kampuni hiyo ipo tayari kuipa ushirikiano   timu ya wataalamu watakaoteuliwa na Rais Dk. John Magufuli kupitia mkataba huo.
Alisisitiza kuwa TanzaniteOne itafanya hivyo kwa vile  inatambua  juhudi na hatua zinazochukuliwa na Rais Dk. Magufuli   kuwezesha madini kuwanufaisha Watanzania na taifa kwa ujumla.
“Septemba 7 mwaka huu, Rais Dk. Magufuli alipokea ripoti ya Kamati ya Bunge iliyochunguza mwenendo wa uchimbaji na biashara ya madini ya Tanzanite.
“Baada ya kupokea, alifika Merereni Septemba 21, mwaka huu ambako alitoa maelekezo mahususi yakiwamo  kupitiwa upya   mkataba wa mgodi unaosimamiwa na Kampuni ya Tanzanite One Mining Limited,” alisema.
Mnzava aliongeza: “Oktoba 19, mwaka huu  baada ya kupokea taarifa ya maendeleo ya mazungumzo baina ya Tanzania na Kampuni ya  Barrick, Rais Dk. Magufuli alitoa  maelekezo kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi kuwa timu ya Serikali ianze kufanyia kazi madini ya Tanzanite na almasi.
“TanzaniteOne itashirikiana bega kwa bega na timu ya Serikali itakayoundwa kwa ajili ya kutekeleza wajibu huo, lengo likiwa ni kuwezesha madini hayo kuwa ya manufaa kwa taifa na watanzania kwa ujumla”.
Alisema kwa kuzingatia maelekezo hayo, TanzaniteOne ipo tayari kuingia kwenye majadiliano na Serikali kufanya mapitio ya mkataba husika.
Mnzava alisema kampuni yake inafanya hivyo kwa sababu kubwa mbili;  mosi, wanatambua juhudi na hatua zinazochukuliwa na Rais Dk. Magufuli kuwezesha madini kuwanufaisha watanzania.
“Pili tunaamini kwamba wabia ambao ni watanzania wazawa katika TanzaniteOne wana wajibu kushiriki katika mchakato wa kuliwezesha taifa kunufaika na rasilimali za madini,” alisema.
Mnzava aliongeza: “Wakati tukisubiri taratibu za Serikali kukamilika kabla ya kuanza mchakato wa majadiliano, tunapenda kumhakikishia Rais Magufuli na Watanzania kwa ujumla TanzaniteOne tutatoa ushirikiano utakaowezesha kuwa na hitimisho lenye tija kwa taifa letu.
Juni, mwaka huu wakati Rais Dk. Magufuli akipokea ripoti ya kamati ya madini iliyoongozwa na Abdulkarim Mruma, aliagiza kukamatwa   wakurugenzi wa TanzaniteOne, Hussein Gonga na Faisal Juma kutokana na kuguswa kwenye ripoti hiyo.
Hata hivyo, siku chache akiwa ziarani Manyara, Rais aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuwaachia huru wawekezaji ‘wenye umuhimu’ katika migodi ya Tanzanite waliokamatwa kwa ajili ya kusaidia kutoa taarifa nyeti.
Aliagiza  wakakae na kamati ya kujadili madini  kurekebisha mkataba utakaokuwa na faida kwa serikali na si wa unyonyaji.
Pia aliagiza  kuanza haraka ujenzi wa ukuta katika eneo lote la vitalu A mpaka D   la ukubwa wa kilomita za mraba 81.99, linalotajwa kuwa na Tanzanite nyingi.

No comments:

Post a Comment