Benki hiyo, First Housing Finance imeanzishwa kwa mtaji wa Sh21.8 bilioni na itakuwa ikitoa mikopo ya kununua, kujenga, kuendeleza au kukarabati nyumba huku mteja akipewa mpaka miaka 20 kulipa deni lake.
Utaratibu huo, licha ya kuwa tofauti na mwenendo wa mikopo ilivyo nchini ambayo benki nyingi hutoa mpaka miaka 15, itakuwa na riba nafuu ili kutoa fursa kwa wengi kumiliki nyumba.
Mkurugenzi mwendeshaji wa benki hiyo, Omar Msangi alisema Benki M kwa kushirikiana na wabia wake imeingia katika soko la mikopo ya nyumba kuleta suluhisho la kudumu kwa Watanzania.
Wabia wengine
Licha ya IFC, wabia wengine wa taasisi hiyo ni familia ya Karimjee na Sanjay Suchak na kampuni inayoongoza katika sekta ya mikopo ya nyumba barani Asia, Housing Development Finance Corporation Limited (HDFC) ya India.
Banki M inamiliki asilimia 40 ya hisa za kampuni hiyo mpya, wakati wabia wake wanne waliobaki wakiwa na asilimia 15 kila mmoja.
Taarifa ya ununuzi wa hisa iliyotolewa na HDFC Juni ilibainisha kununua hisa milioni 32.7 ambazo ni asilimia 15 kwa Dola 1.5 milioni za Marekani. Kampuni hiyo iliyoorodheshwa katika Soko la Hisa Bombay (BSE), ilisema inataka kuimarisha mikopo ya nyumba Tanzania ambako taasisi nyingi za fedha hazijaipa kipaumbele.
Mikakati ya Serikali
Mwaka 2011, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliridhia kuanzishwa kwa Shirika la Mikopo ya Nyumba (TMRC) linalozikaribisha benki za biashara na taasisi nyingine za fedha kuwa wanachama ili ipate mikopo nafuu kwa ajili ya kuwakopesha wateja wake. Kila mwanachana, anatakiwa kununua hisa zenye thamani isiyopungua Sh500 milioni.
Tangu lianzishwe mpaka sasa, shirika hilo lenye zaidi ya benki 20 wanachama linaendelea kuweka mazingira rafiki kwa Watanzania kumiliki nyumba za kudumu kwa gharama ya chini iwezekanavyo.
Kuanzishwa kwa First Housing Finance iliyopewa leseni ya BoT Julai 18 ili ianze kutoa huduma nchini, kutaongeza ushindani kwenye sekta hiyo hivyo kushusha riba. Kampuni hiyo inaanza ikiwa na tawi moja jijini Dar es Salaamhuku uongozi ukisema mipango inaandaliwa kufungua mengine mikoani.
No comments:
Post a Comment