Tuesday, October 31

SWEDEN YATOA BILIONI 80/- KUCHANGIA MAENDELEO TANZANIA


UBALOZI wa Sweden nchini, umewekeana saini makubaliano na Umoja wa Mataifa na utatoa Sh bilioni 80.4 kwa shughuli za maendeleo ndani ya miaka minne.
Baada ya kutiliana saini, Balozi wa Sweden nchini, Katarina Rangnitt, alisema wamechagua kusaidia shughuli za Umoja wa Mataifa zinazoakisi malengo ya maendeleo ya nchi katika nyanja za haki za wanawake, utawala wa demokrasia na ukuaji wa uchumi.
Alisema shughuli hizo ni zile ambazo  zinamnufaisha kila mmoja katika kipindi ambacho Tanzania inalenga kuwa na uchumi wa kipato cha kati.
“Kwa kupitisha sehemu ya msaada wetu kupitia Mfuko wa Umoja wa Mataifa chini ya mpango wa kufanya kazi pamoja, tunashiriki kikamilifu katika kusaidia ufikiwaji wa malengo ya maendeleo nchini Tanzania.
“Vile vile tunatambua bayana kabisa na kuthamini wajibu waliokubaliwa kuwa ndio wa Umoja wa Mataifa katika kuleta maendeleo endelevu,’’ alisema  Rangnitt.
Aliongeza kuwa kwa msaada huo wanawezesha uchukuaji unaoendana na sera ya nje inayozingatia haki za wanawake wa Sweden na pia jitihada  zinazolenga  ajira yenye hadhi na haki za watoto.
Aidha alisema wapo tayari kuendelea kuisaidia Tanzania na Umoja wa Mataifa pamoja na kuyapokea mageuzi ya mfumo wa UN chini ya mpango wa kufanya kazi pamoja na kutambua njia fungamanifu zinazotumika na thamani inayopatikana kutokana na mchango wa mashirika ya UN katika kushirikiana na Tanzania.
Mratibu  Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi Mkazi wa UNDP , Alvaro  Rodriguez, alishukuru msaada huo endelevu  na kuipongeza Sweden kwa kuwa mshirika wa maendeleo asiyeyumba katika shughuli za UN na Tanzania.

No comments:

Post a Comment