Tuesday, October 31

MITA 60 BONDE LA MTO RUFIJI ZATESA WANANCHI


WATAALAMU wa Bonde la Mto Rufiji wamelalamikiwa kwa kushindwa kutoa elimu kwa wananchi wa Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe ili kufahamu sheria inayokataza watu  wasifanye shughuli za kibinadamu mita 60 kutoka kwenye vyanzo vya maji.
Akizungumza wakati wa operesheni ya kuondoa mabomba ya maji yaliyowekwa na wananchi wanaofanya kilimo cha umwagiliaji pembezoni mwa bonde hilo, Diwani wa Kata ya Imalinyi, Onesmo Lyandala, alisema kama wananchi wake wangeelimishwa sheria za mita 60 wasingefanya kilimo hicho.
Operesheni hiyo ilitekelezwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Wanging’ombe ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya, Ali Kassinge na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Wanging’ombe (WANGIWASA).
“Mpaka sasa operesheni hii imekata miti, mabomba ambayo yalikuwa yakitumika katika kumwagilia, tumeichukua na itakua ni mali ya kijiji.
“Hata hivyo, hakuna mwananchi anaifahamu sheria ya mita 60 zinaanzia wapi na kuishia wapi, ”alisema Lyandala.
Mtaalamu wa Maji Bonde la Mto Rufiji, Abisai Chilunda, alisema hatua ya kuharibu miundombinu ya mabomba kwenye vyanzo vya maji katika bonde hilo, imetokana na usimamizi wa sheria namba 11 ya mwaka 2016 kuhusu rasilimali za maji.

No comments:

Post a Comment