Polisi wataka kumkamata, wafeli, IGP Sirro akerwa kuulizwa upelelezi wa tukio hilo, Chadema wamjibu
Waandishi Wetu
TUKIO la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, kupigwa risasi, limechukua sura mpya baada ya polisi kutaka kumkamata Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda.
Ponda alinusurika kuingia mikononi mwa polisi jijini Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kile alichoambiwa na mbunge huyo jijini Noirobi alipoenda kumjulia hali.
Polisi walivamia ukumbi ambao Ponda alikuwa anafanya mkutano kwa nia ya kumkamata, lakini hawakufanikiwa baada ya kukuta kiongozi huyo tayari ameshaondoka eneo hilo.
Baada ya kumkosa kiongozi huyo, polisi waliwachukua baadhi ya waandishi wa habari na kuwapeleka Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam (Central) na baadae kuwaachia.
Alichosema Ponda
Sheikh Ponda alisema hivi karibuni alikuwa nchini Kenya kumjulia hali Lissu ambapo ajenda yake ilikuwa ni kumwombea dua, kumjengea matumaini ya afya yake, kujenga mazingira endelevu ya harakati zake kwa umma na kujenga mazingira ya kuzungumzia tukio lililomkuta mbunge huyo.
Alisema baada ya kuonana na Lissu, ameona anaendelea vizuri na kwamba ameahidi pindi atakapopona atarudi nchini kwa ajili ya kutetea maslahi ya umma.
Ponda alisema kwa sasa vitendo vya uhalifu wa utekaji, mauaji, vitisho vya kuawa vimezidi, jambo linalosababisha wananchi kupata hofu.
Alisema, imefika wakati wananchi wanapaswa kushirikiana kupiga kelele juu ya vitendo hivyo ambavyo vinachangia watu wasio na hatia kuuawa.
“Ninawaomba wanasiasa, wasomi, viongozi wa dini mbalimbali tushirikiane pamoja na kujitokeza hadharani ili kukemea vitendo vya uhalifu wa utekaji au mauaji yanayofanywa na kikundi cha watu wasiojulikana.
“Ifike wakati tuseme sasa basi, inatosha katika hili… na mimi nitakuwa mstari wa mbele kujitokeza hadharani na kukemea,” alisema Ponda.
Alisema anaamini kitendo cha kujitokeza hadharani, kutasaidia kuiamsha Serikali na kuona kuwa wananchi wamechoka na vitendo viovu vikiwamo vya utekaji na mauaji vinavyofanywa na watu wasiojulikana.
“Mimi mwenyewe mwaka 2013 nilipigwa risasi, mwaka huu tena amepigwa Lissu, ninawaomba wananchi tujitokeze ili kukemea kwa sababu havikubaliki,”alisema.
Alisema kauli yake siyo ya kichochezi, ila inategemea mtu atakayetoa tafsiri kuhusu kauli hiyo na kama anaona anachochea.
“Kauli inaweza kutafsiriwa kwa aina nyingi, wapo watakaosema nimekuja kuchochea na wapo watakaoona nipo sahihi, lakini kwa sababu vyombo vya kutafsiri kauli vipo, wao ndiyo watakaotoa uamuzi wa kauli yangu nimechochea kwa kivipi,”alisema.
Sirro akerwa kuulizwa upelelezi wa Lissu
Akiwa mkoani Iringa, Sirro alionyesha kukerwa na kuulizwa maswali juu ya upepelezi wa Lissu kila wakati na kusema, tukio lake ni la kawaida sawa na matukio mengine na kwamba upelelezi wake unaendelea.
“Mimi si mwanasiasa, hili ni tukio kama yalivyo matukio mengine na Lisu ni Mtanzania kama wengine, hivyo Jeshi la Polisi linaendelea kulifanyia uchunguzi suala hilo kama yalivyo matukio mengine.
“Kila siku maswali ni juu ya Lissu, ila niwaambie kuwa hili ni tukio kama matukio mengine tunaendelea na uchunguzi,” alisema Sirro.
Alisema suala la Lissu limekuwa likizungumzwa kila wakati na kwamba ifahamike kuwa suala hilo linafanyiwa kazi na kitengo cha upelelezi na hategemei kufundishwa kazi na mtu juu ya nini afanye katika suala hilo .
Chadema wambana Sirro
Mwanasheria wa Chadema, John Mallya, alisema kauli iliyotolewa na Sirro hivi karibuni ya kuwataka wananchi kutojadili suala la kupigwa kwa Lissu ipuuzwe kwa sababu hakuna sheria inayotakaza kujadili suala hilo.
“Katiba Ibara ya 18 inatoa uhuru kwa raia kupashana habari na uhuru. Kamanda Sirro hana mamlaka ya kuamuru wananchi kwenye sheria wala katika kanuni na kwamba wananchi wanyamaze ni kinyume cha masharti ya ibara hiyo na anatufanya tukose imani na Jeshi la Polisi.
“Mtu wa kunyamaza hapa ni Kamanda Sirro, ili afanye kazi ya upelelezi, anapaswa kuchukua fursa kwa majadiliano yanayoendelea, na watu hawawezi kumpelekea ushahidi bila kujadiliana kwanza,” alisema.
Alisema Kamanda Sirro anaongozwa na sheria kadhaa lakini kubwa anaongozwa na sheria ya Jeshi la Polisi na huduma saidizi, msaafu anaotumia unaitwa ‘Police General Order’ (PGO) kwenye Jeshi la Polisi hii ni sheria maarufu sana wao wenyewe wanaijua ndiyo inasema IGP anamuamuru nani na nani hawezi kumuamuru.
“Namkumbusha IGP Sirro kuwa yeye ni Kamanda wa Polisi na si kamanda wa raia hana mamlaka ya kutoa amri wananchi wajadili nini na nini wasijadili mamlaka hayo hana,” alisema.
Ponda alivyowapiga chenga polisi
Licha ya polisi kuvamia mkutano huo wa Ponda jana, hawakufanikiwa kumpata kiongozi huyo na badala yake wakaondoka na baadhi ya waandishi wa habari.
Hata hivyo haikujulikana haswa lengo lao la kutaka kumkamata Sheikh Ponda.
Askari hao walifika saa 4:45 asubuhi katika hoteli moja iliyopo Kariakoo ambayo Sheikh Ponda alikuwa akifanyia mkutano huo wakiwa kwenye magari mawili.
Muda wanafika eneo hilo, ilikuwa ni dakika chache tangu Sheikh Ponda kuondoka eneo hilo baada ya kumaliza mkutano wake.
Ponda alifika kwenye hoteli hiyo saa 3:45 asubuhi na kuwasubiri waandishi na saa 4:10, alianza mkutano wake ambapo alitumia wastani wa dakika 20.
Mara baada ya kuondoka, polisi hao walivamia mkutano huo na kuwazuia waandishi wa habari kutoka ndani ya ukumbi huo hadi watakapompata Sheikh Ponda.
Baadhi ya askari walifanya ukaguzi wa hoteli nzima ili kuangalia kama amejificha au laa, huku wengine wakiwa wamebaki na waandishi kwenye ukumbi ambao mkutano huo ulifanyika.
“Hakuna mwandishi yeyote kutoka ndani ya hoteli hii mpaka tumpate Sheikh Ponda, mliopo ndani hakuna kutoka,” alisikika askari mmoja akiwaambia waandishi wa habari.
Baada ya kufanya ukaguzi huo na kushindwa kumpata Sheikh Ponda, polisi waliwaruhusu baadhi ya waandishi kuondoka katika hoteli hiyo huku wengine wakiambiwa waende Central kwa ajili ya mahojiano.
Mwandishi wa Blog ya Z4, Ahmed Kombo ni miongoni mwa waandishi walioenda kituo cha polisi kwa mahojiano.
Akizungumza na MTANZANIA, mara baada ya kuachiwa, Kombo alisema, baada ya kufika polisi, walimwambia aandike maelezo ya kilichojiri kwenye mkutano huo pamoja na kuwapa ‘press release’ iliyotolewa na Sheikh Ponda wakati wa mkutano wake.
“Wakati wananipakiza kwenye difenda, mpiga picha wa magazeti ya The Guardian, Seleman Mpochi alikuwa anapiga picha ya tukio, askari mmoja alimfuata na kumpokonya kamera na kumpakiza kwenye difenda.
“Mimi nilipelekwa kituo kikuu cha polisi na Mpochi alipelekwa Msimbazi,”alisema Kombo.
“Niliwapa ile ‘press release’ pamoja na kuandika maelezo ya kilichotokea kwenye mkutano, nilipomaliza waliniachia nikaondoka,”alisema.
No comments:
Post a Comment