Ponda amesema hayo baada ya kumtembelea Lissu aliyelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alikopelekwa baada ya kushambuliwa kwa takriban risasi 30 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake mjini Dodoma katika tukio lililotokea mchana Septemba 7.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini hapa ulioishia kwa baadhi ya waandishi wa habari kukamatwa na Jeshi la Polisi, Sheikh Ponda alisema safari yake ya Nairobi ilikuwa na malengo manne.
Aliyataja madhumuni hayo kuwa ni kumjulia hali Lissu, kumuombea dua na kumjengea matumaini ya afya yake, kumjengea matumaini endelevu ya harakati zake za umma na kujenga mazingira ya kutosha kuzungumzia tukio hili.
“Katika kipengele cha tatu, tulipokuwa tunapeana na kubadilishana hoja, nilipata hisia nzito kwake,” alisema Sheikh Ponda.
“Maana yeye aliye kitandani alinipa mimi matumaini makubwa. Alisema anaamini yuko karibu kurudi jukwaani na ataanzia pale atakapokuta kasi ya mabadiliko imefikia.
“Alinieleza kazi muhimu za kuwajenga watu anazofanya akiwa pale kitandani. Alinieleza anaamini damu yake na yangu na nyingine zitakazomwagika kwa namna hii, zitawafanya Watanzania kupata uhuru wa kweli wenye thamani.”
Sheikh Ponda alisema tukio hilo na mengine ambayo yamekuwa yakitokea nchini yawe funzo na kuifanya jamii kujenga umoja na ushirikiano katika kulirudisha Taifa katika njia sahihi.
“Izingatiwe kwamba ikiwa tatizo lipo na watu hawasemi kama lipo, basi litaendelea kuwepo na wasababishaji pia wataendelea kudumu,” alisema.
“Na wale wanaoamini hali iliyopo ni kwa Serikali kushindwa kutekeleza wajibu wake, tuunganishe nguvu kuhakikisha Serikali inatekeleza wajibu huo.
“Masheikh, maaskofu, mapadri, wana vyuo, viongozi wa upinzani na hata viongozi wazuri walioko CCM waiambie ukweli Serikali. Kimya chao ni hasara na kitawanyima hadhi ya anuwani yao.”
Sheikh Ponda alisema kwa kipindi cha hivi karibuni kumekuwapo na matukio ambayo kwa namna moja au nyingine yanalichafua Taifa katika uso wa kimataifa.
Aliyataja matukio hayo kuwa ni mauaji ya kutisha, maiti za watu kuokotwa kwa wingi na zinaendelea kuokotwa, raia na viongozi kadhaa wametekwa na kupotea, viongozi mashuhuri wa vyama vya siasa vya upinzani na wa taasisi za kidini wanashambuliwa kwa silaha nzito kwa lengo la kuuawa.
Alisema kwa kuwa roho za Watanzania hivi sasa ziko juu na baadhi wamepoteza matumaini ya usalama wao, ni jukumu la Serikali kuhakikisha usalama wa raia wake unakuwapo wakati wote.
Kukamatwa waandishi
Mara baada ya mkutano huo uliofanyikia Hoteli ya Iris iliyopo Mtaa wa Livingstone Kariakoo kumalizika, na waandishi kadhaa kuondoka, askari wa Jeshi la Polisi walifika kumfuata Sheikh Ponda.
Askari hao waliokuwa wamevalia kiraia na wengine sare, walikuwa kwenye gari mbili na kuzuia mtu yeyote kutoka huku wakitaka kujua alipo Sheikh Ponda na walipoelezwa kwamba ameshaondoka, walianza kumsaka.
“Tulipowaeleza kwamba kaondoka walianza kutuomba material ya kile alichozungumza Sheikh Ponda. Mimi nilikubali na tukaanza kushuka kwenda katika gari lao,” alisema Rashid Kombo, mwandishi wa Z4News. “Wakati tunashuka na kwenda kupanda katika gari lao, mpiga picha wa Nipashe, John Badi akawa anapiga picha. Walipomwona wakamchukua na tukaondoka naye.
“Tulipofika Central (kituo kikuu cha polisi) wakanishusha mimi kwenda kuwapa material na Badi wakaondoka naye kumpeleka kituo cha Msimbazi na mimi nilipomaliza kuwapa material wakaniachia.”
Alipotafutwa na Mwananchi, Badi alisema alihojiwa kuhusu tukio hilo na baadaye kuachiwa.
“Mimi baada ya kufika pale Iris Hotel na kukuta magari ya polisi nilijiuliza kuna nini. Ndipo nikatoa kamera na kuanza kupiga picha na ndipo waliponichukua mimi na mwenzangu Suleiman Mpochi hadi Msimbazi,” alisema Badi.
“Tulivutana nao wakiuliza kwa nini tunapiga picha askari wakiwa kazini. Sisi tukawaeleza tatizo lipo wapi. Mwisho wa siku walituachia.”
Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa hakupatikana kuzungumzia tukio hilo na Mwananchi ilipomtafuta Kaimu Kamanda wa Polisi Ilala, Joseph Matuki alisema hakuwa na taarifa hizo.
“Hizo taarifa kwanza ndiyo unanipa wewe, sikuwa najua kama Sheikh Ponda alikuwa na mkutano hapo Iris.” alisema.
Alipoulizwa inawezekana polisi wakaenda pale bila yeye kujua, Kamanda Matiku alisema “kama wametumwa na bosi mimi nitaajuaje”, lakini hakutaja ni bosi gani.
No comments:
Post a Comment