Thursday, October 12

Magufuli, Aga Khan wazungumzia mambo matatu

Rais John Magufuli akimpokea Imamu wa Waislamu
Rais John Magufuli akimpokea Imamu wa Waislamu wa Shia Ismailia duniani, Mtukufu Aga Khan alipowasili Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Mtukufu Aga Khan ameanza ziara ya siku mbili nchini ikiwa ni mwaliko wa Rais Magufuli. Picha na Ikulu 
Dar es Salaam. Rais John Magufuli na Kiongozi wa madhehebu ya Ismailia duniani, Mtukufu Aga Khan wamezungumzia mambo matatu yatakayosaidia maendeleo ya Tanzania.
Mambo hayo ambayo yaliwekwa wazi na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ni sekta ya afya, elimu na vyombo vya habari.
Katika mazungumzo yao yaliyofanyika Ikulu jana Mtukufu Aga Khan alimweleza Rais Magufuli kwamba taasisi yake imedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kupanua Hospitali ya Aga Khan iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mtukufu Aga Khan aliwasili nchini jana kwa ziara ya siku mbili akitokea Uganda ambako alihudhuria sherehe za Uhuru wa nchi hiyo kwa mwaliko wa Rais Yoweri Museveni. Baada ya kuwasili, alikwenda moja kwa moja Ikulu na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli.
Katika mazungumzo yao, Mtukufu Aga Khan alimweleza Rais Magufuli kwamba upanuzi wa Hospitali ya Aga Khan utahusisha kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa kutoka 72 vya sasa hadi kufikia 172.
Pia, alimweleza kuwa itaimarisha matibabu ya moyo na kansa na kuongeza ufundishaji wa madaktari na wataalamu wengine wa afya.
Akizungumza baada ya mazungumzo yao, Rais Magufuli alimshukuru Mtukufu Aga Khan kwa jinsi taasisi zake zinavyotoa huduma za kijamii hapa nchini, lakini akatoa wito kwa taasisi hizo kupunguza gharama za huduma zake kwa wananchi ili waweze kumudu.
“Wanatoa huduma nzuri na mimi kwa niaba ya Watanzania na Serikali kwa ujumla nimeshukuru sana, nimemshukuru sana mzee Aga Khan na watu wake wote kwa kazi kubwa wanazozifanya kwa ajili ya Watanzania,” alisema Rais Magufuli.
Alisema “wame-create (wametengeneza) employment (ajira), wamefanya mambo makubwa. Kwa mfano, kwenye hospitali wanatoa training (mafunzo) ya bure, nafikiri kila mwaka huwa wanatoa watu karibu 100 kwa ajili ya kuwafanyia training.”
Rais Magufuli alisema Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na Aga Khan na alimuomba kiongozi huyo kuendelea kupanua wigo wa huduma za taasisi zake ikiwa ni pamoja na kuwekeza mjini Dodoma yaliko makao makuu ya Serikali.
Elimu
Kuhusu elimu, Rais Magufuli alisema Mtukufu Aga Khan na taasisi yake wataanzisha ujenzi wa chuo kikuu kikubwa huko Arusha na tayari wameshapata eneo. Rais Magufuli alisema Mtukufu Aga Khan alimweleza kwamba ujenzi huo utaanza ndani ya miezi sita.
Kama ilivyokuwa katika afya, pia Rais alisema kuna changamoto chache ambazo ni bei kubwa katika huduma za elimu zinazotolewa na taasisi za Aga Khan lakini akasema Mtukufu Aga Khan ameahidi kulishughulikia suala hilo na tayari ameshatoa maelekezo kwa watu wake.
Vyombo vya habari
Baada ya mazungumzo na Rais Magufuli, Mtukufu Aga Khan alisema haamini kwamba kipaumbele cha vyombo vya habari ni kujikita kwenye habari za siasa pekee, badala yake alisema anaamini vyombo hivyo vina wajibu mpana zaidi wa kujikita katika masuala ya maendeleo hususan katika nchini zinazoendelea.
Alisema taasisi ya Aga Khan ipo katika mchakato wa kujikita katika wajibu huo kwa kuwa na waandishi wa habari na wachambuzi mahiri waliobobea katika fani mbalimbali licha ya kwamba hilo linachukua muda mrefu kuwaandaa.
“Tunahitaji weledi kwenye hii tasnia. Tunahitaji watu wanaoweza kuzungumzia mambo ya afya; wanaoweza kuzungumzia uchumi; wanaoweza kuzungumzia masuala ya dini; wanaoweza kuzungumzia siasa wanaoweza kuchangia kwenye mambo ya Katiba. Tunahitaji yote haya,” alisema Mtukufu Aga Khan
Kuhusu AKDN
Mtukufu Aga Khan pia ni kiongozi wa mtandao wa maendeleo wa Aga Khan (AKDN) ambao unatoa huduma mbalimbali duniani.
Kwa hapa nchini, mtandao huo unatoa huduma za afya, bima, elimu, mikopo kwa wajasiliamali na kusaidia kilimo hasa kwa wakulima wa vijijini.
Ziara ya Aga Khan inalenga kuimarisha ushirikiano baina ya serikali na taasisi yake ambayo ina uwekezaji mkubwa hapa nchini ambazo ni pamoja na sekta ya afya, elimu, mawasiliano, taasisi za fedha na viwanda.

No comments:

Post a Comment