Wednesday, October 11

Salma Kikwete awafunda watoto wa kike kukwepa mimba za utotoni

Mke wa rais mstaafu Mama Salma Kikwete akikagua
Mke wa rais mstaafu Mama Salma Kikwete akikagua shughuli zinazofanywa na shirika la room to read wakati wa maadhimisho ya siku mtoto wa kike uwanja wa bwawani mailimoja mjini Kibaha. Picha na Julieth Ngarabali 
Kibaha. Mbunge wa Kuteuliwa, Salma Kikwete amewataka watoto wa kike  kutambua thamani ya msichana ni kufunga mapaja na kuyazuia.
Amesema kwa kufanya hivyo hakuna mdudu yoyote atakayeingia katikati ya mapaja yao.
Salma ambaye ni mke wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete ametoa ujumbe huo mjini Kibaha leo Jumatano wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike mkoani Pwani, katika viwanja vya bwawani Maili Moja.
Amesema wasichana wasione haya kuwaambia wanaume wakware kuwa wao ni lulu, na thamani ya lulu ni usichana wao ambao utakuwepo tu pale wanapofunga mapaja.
"Msichana funga mapaja yako sasa, zuia kabisa mapaja yako maana ukizuia hakuna mdudu atakayeingia katikati ya mapaja hayo. Tumeelewana watoto," amesema akiwahoji waliohudhuria maadhimisho hayo.
Ameshauri kuwa, ni vyema watoto wakakubaliana na mazingira ya wazazi kwamba, wakiwa shule wasitake kuwa na mashati matatu.
Amewaasa wasitake kuwa na fedha ya chipsi au kuwa na viatu pea mbili bali waridhike na hali za wazazi wao ili wasije kupata mimba za utoto.
“Nalazimika kutumia lugha hii nyepesi ili watoto wote wanielewe ninachomaanisha  kirahisi itaweza kusaidia kuliko kutumia lugha ngumu watakuwa wanaulizana anamaanisha nini, na sitaki wabaki na swali bali waelewe kabisa," amesema Salma.
Kuhusu wanaume wakware, Salma amewataka kuachana na mabinti kwa kuwa wapo watu wazima mtaani wakawatafute hao na si wanafunzi.
Amesema changamoto zinazowakabili watoto wa kike haziwezi kutatuliwa na Serikali peke yake au na shirika la Room to read, bali na wananchi wote kwa kushikamana, kujenga nguvu na sauti ya pamoja.
Salma amewataka wenyeji wa Pwani kupinga mimba za utoto kwa kuwa mkoa huo upo katika orodha ya mikoa 10 yenye changamoto ya mimba za utotoni
Amesema ni vizuri mkoa kuongoza kwa mambo mazuri ya maendeleo na si mimba hizo.
Mkoa wa Pwani unatajwa kuwa na asilimia 30 ya mimba za utotoni, huku Katavi ukiongoza kwa asilimia 45.

No comments:

Post a Comment