Wednesday, October 11

Mawaziri Hispania wakutana kuijadili Catalonia


Madrid, Hispania. Waziri mkuu wa Hispania Mariano Rajoy leo amechukua hatua ya kwanza kuelekea kutekeleza ibara ya 155 ya katiba, ambayo itamruhusu kusimamisha mamlaka ya kisiasa ya Catalonia na kisha kulitwaa eneo hilo. 
Kikao hicho cha dharura kimefanyika siku moja baada ya Rais wa Catalonia, Carles Puigdemont kutia saini hati ya kujitenga ingawa alisitisha kutangaza uhuru kamili kutoa fursa ya kufanya mazungumzo katika ngazi ya kitaifa na ile ya kimataifa.
Puigdemont alisema jana kwamba ataendelea na mchakato wa kujitenga lakini anasitisha kwa siku kadhaa. Wakati Puigdemont akivuta subira kutoa nafasi ya mazungumzo, Serikali Kuu ya Madrid imeonyesha kuwa hakuna uwezekano huo.
"Baraza la Mawaziri limeamua kuitaka rasmi Serikali ya Catalonia kuthibitisha kama kweli imejitangazia uhuru au la,” amesema Rajoy alipohutubia kupitia televisheni.
"Majibu kutoka kwa rais wa Catalonia yatatusaidia kufanya maamuzi ya matukio mengine yanayofuata, katika siku chache zijazo," alisema na kuongeza kwamba ataendelea kuchukua hatua kwa njia ya “tahadhari na uwajibikaji.”
Masharti hayo maalumu yatahitajika ili kuanzisha mchakato wa matumizi ya ibara ya 155 ingawa katiba haijaweka kipindi fulani cha muda wa kupata jibu. Kutekeleza ibara hiyo ya 155, serikali kuu inaweza kuchukua baadhi ya mikoa 17 au yote ikiwa hawatatimiza masharti ya kisheria.
Pengine kutokana na shinikizo kutoka pande zote, pamoja na Ulaya, Puigdemont aliyeahidi kubadilisha Catalonia kuwa "Jamhuri" huru amesitisha mchakato huo akisubiri kupata "ufumbuzi" katika mazungumzo na serikali kuu ya Madrid.

No comments:

Post a Comment