Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 25 Oktoba, 2017 amepokea hati za utambulisho za Mabalozi watatu waliopangiwa kuziwakilisha nchi za Oman, Uholanzi na China hapa nchini.
Waliowasilisha hati zao kwa Mhe. Rais Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Mhe. Ali Abdullah Al Mahruqi – Balozi wa Oman hapa nchini, Mhe. Jeroen Verheul – Balozi wa Uholanzi hapa nchini na Mhe. Wang Ke – Balozi wa China hapa nchini.
Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Mabalozi hao kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao hapa nchini na amewahakikishia kuwa Serikali yake itafanya kazi nao kwa ukaribu ili kuendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya nchi hizo na Tanzania hususani katika uchumi.
“Nimefurahishwa sana na ziara iliyofanywa na Mawaziri wa Oman hapa nchini, naomba ufikishe shukrani zangu kwa Mfalme wa Oman Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said, naamini yote tuliyozungumza ikiwemo kubadilishana uzoefu katika mafuta na gesi, uwekezaji katika viwanda na ujenzi wa miundombinu tutayatekeleza kwa manufaa ya wananchi wa nchi zetu” amesema Mhe. Rais Magufuli alipozungumza na Balozi Ali Abdullah Al Mahruqi wa Oman.
Mhe. Rais Magufuli amemuambia Balozi Jeroen Verheul wa Uholanzi kuwa Tanzania inayo gesi nyingi na itafurahi kupokea wawekezaji kutoka Uholanzi ikizingatiwa kuwa nchi hiyo ina uzoefu na teknolojia kubwa katika sekta hiyo.
Kwa upande wa Balozi wa China hapa nchini Mhe. Wang Ke, Mhe. Rais Magufuli amesema uhusiano wa Tanzania na China ni wa kihistoria na kidugu, hivyo ametoa wito kwa Balozi huyo kuuendeleza na kuhakikisha fursa zenye manufaa kwa nchi zote zinatumiwa ipasavyo ikiwemo kukuza uwekezaji, biashara, utalii na ushirikiano katika usafiri wa anga.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Dar es Salaam
25 Oktoba, 2017.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi wa China hapa nchini Wang Ke, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China hapa nchini Wang Ke akijitambulisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akitazama vitabu alivyokabidhiwa na Balozi wa China hapa nchini Wang Ke, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China hapa nchini Wang Ke akiwa amesimama wakati wa nyimbo za Mataifa ya China na Tanzania zikipigwa katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati ya utambulisho kutoka kwa Balozi wa Uholanzi hapa nchini Jeroen Verheul Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimpongeza Balozi wa Uholanzi hapa nchini Jeroen Verheul mara baada ya kupokea Hati zake za Utambulisho Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akipokea Hati ya Utambulisho kutoka kwa Balozi wa Oman hapa nchini Ali Al Mahruqi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Oman hapa nchini Ali Al Mahruqi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika mazungumzo na Balozi wa Oman hapa nchini Ali Al Mahruqi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Oman hapa nchini Ali Al Mahruqi akiwa amesimama wakati wa nyimbo za mataifa mawili ya Oman na Tanzania zikipigwa mara tu baada ya kuwasili katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA NA IKULU
No comments:
Post a Comment