Tathmini hiyo iliyochapishwa na Jarida la Afya la Lancet na kufadhiliwa na Taasisi ya Bill and Melinda Gates, imebaini hakuna nchi hata moja kati ya 200, ikiwamo Tanzania zilizofanyiwa tathmini zilizoweza kufikia malengo ya Umoja wa Mataifa (UN) katika kutokomeza maambukizi mapya ya kifua kikuu na Ukimwi ifikapo 2030.
Kadhalika, tathmini hiyo iliyochapishwa Septemba 12, imebaini chini ya asilimia tano tu ya nchi hizo ndizo zinazoonekana zitafikia malengo hayo ya UN ya kukabiliana na matukio ya kujiua, ajali za barabarani na unene kupita kiasi kwa watoto ifikapo 2030.
Pia ni asilimia saba tu ya nchi hizo ndizo zinazoweza kumaliza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Imeelezwa kwa ujumla ni asilimia tano tu ya malengo 37 yaliyowekwa chini ya Mpango wa Maendeleo Endelevu ya UN(SDG) ya 2015, ndiyo yanayotarajiwa kufikiwa.
Mwandishi wa utafiti huo ameandika idadi kubwa ya malengo bado inaonekana haitafikiwa na nchi wanachama wa UN.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Bill and Melinda Gates, Anitha Zaidi anasema nchi za Afrika hata hivyo zimepiga hatua kubwa tangu 1990 katika kupunguza vifo vya watoto.
“Mpaka sasa tumepunguza kwa karibu asilimia 50. Lakini bado kuna watoto milioni sita wanafariki dunia kila mwaka na idadi kubwa wanatoka Afrika.
Mzigo mkubwa upo Afrika kwa sasa na baadhi ya maeneo ya Asia, lakini kwa Afrika kuna tatizo zaidi na endapo hatutachukua hatua zaidi, hatutaweza kufikia malengo endelevu ya UN,” anasema.
Hata hivyo, anasema kama hakutakuwa na dhamira ya dhati ya kuendelea mbele na kuwaangalia walio maskini na kuwapa chanjo, huduma bora za afya, chakula, huduma za uzazi salama, kutoa chanjo na kama hawatafanya juhudi za ziada, malengo hayo ni ndoto kufikiwa.
Utafiti huo pia ulihusisha watafiti 2,500 duniani kote na uliangalia nchi 188 na malengo yao waliyoyaweka kufikia 2030.
Malengo ya nchi hizo yalikuwa ni pamoja na kuwa na hatua mpya za uharakishaji na uimarisha wa huduma za afya, pia kupunguza madhara na kupanua huduma muhimu za afya kwa nchi zote.
Kadhalika, jopo hilo la watafiti lilibaini matabaka katika malengo yaliyowekwa kati ya nchi maskini na tajiri.
Kwa mfano nchi zenye kipato cha juu, zilijitabiria kufikia asilimia 38 ya malengo ya afya ya UN ukilinganisha na asilimia tatu kwa nchi maskini.
Pia nchi hizo hazikuwa zikifanyia kazi matatizo yanayofanana.
Tathmini hiyo pia imebaini kuwa nchi maskini zilifanya vibaya katika suala la vifo vya uzazi, udumavu wa watoto, malaria na madhara ya kimazingira vitu ambavyo huathiri nchi tajiri kwa kiwango kidogo.
Lakini lilipokuja suala la mtindo wa maisha, nchi zenze kipato cha juu ikiwamo Marekani, zilifanya vibaya kwenye suala la kesi za kujiua, matumizi mabaya ya pombe na mauaji.
Hata hivyo, watafiti katika tathmini hiyo wamesema juhudi za kupambana na malaria, vifo vya watoto wachanga na wajawazito zimeonekana, kwani asilimia 60 ya nchi zimeonekana zitaweza kufikia malengo hayo ya UN.
Jopo hilo la watafiti limesema kwa sasa nchi kama za Kazakhstan, Timor-lester, Angola, Nigeria na Swaziland zimetabiriwa kuwa na maendeleo mazuri katika kufikia malengo hayo kutokana na kuonyesha mafanikio hasa katika kupunguza vifo vya watoto, upatikanaji wa afya bora, uzazi wa mpango na huduma za uzazi.
Kwa mujibu wa tathmini hiyo, nchi za Sri Lanka, Venezuela, Serbia na Ukraine zinaonekana kufeli kabisa katika malengo hayo hasa katika unene kupita kiasi na matumizi mabaya ya pombe.
Ripoti hiyo namesema China na Cambodia ni miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kati na wa chini, zinahitajika kutambuliwa kwa kufaulu katika kuimarisha maisha ya wakazi wake.
Kadhalika, Rwanda, Equatorial guinea, Lagos, na Uturuki, zimejiimarisha zaidi kwenye utoaji wa huduma za afya kati ya 2000 na 2016.
Huduma walizozitoa ni pamoja na utoaji wa chanjo, kupunguza vifo vya watoto na maambukizi ya malaria.
Kwa upande mwingine, Marekani, Lesotho na Jamhuri ya Afrika ya Kati ni miongoni mwa nchi zilizoonyesha maendeleo ya chini katika huduma za afya kwa wananchi wake.
Suala la huduma za afya kwa wananchi nchini Marekani lina mjadala mkubwa baada ya uongozi wa Rais, Donald Trump kutaka kuuondoa mfumo wa huduma za afya ulioasisiwa na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Barrack Obama, maarufu kama Obama care.
Marekani pia imetajwa kushika namba 24 kwa kufanya vibaya katika kukabiliana kesi za kujiua, udhalilishaji wa watoto, matumizi mabaya ya pombe na mauaji.
Pia, Singapore, Iceland na Sweden zimetajwa kufanya vizuri katika masuala ya afya.
Kwa upande mwingine, Somalia, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Afghanistan zilifanya vibaya zaidi katika masuala ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wake.
Hata hivyo, China ilipata alama ndogo kwenye kukabiliana na uchafuzi wa mazingira, ajali za barabarani, matumizi ya sumu na uvutaji wa sigara.
India ilishika nafasi ya 127 baada ya kufanya vibaya katika kesi za uchafuzi wa mazingira na utapiamlo kwa watoto.
No comments:
Post a Comment