Mhasibu mmoja nchini Italia amefungwa jela miaka 24 kwa kuwaambukiza makusudi wanawake 30 virusi vya Ukimwi.
Valentino Talluto anadaiwa kushiriki mapenzi bila kinga na wanawake angalai 53 baada yake kupatikana na virusi vya Ukimwi mwaka 2006, mwanamke mdogo zaidi miongoni mwa hao alikuwa na miaka 14 wakati wa kuanza uhusiano wao.
Mhasibu huyo ambaye alikuwa anatumia lakabu "Hearty Style", alitumia mitandao ya kijamii na tovuti za kuchumbiana kuwawinda waathiriwa wake.
Ijumaa, jaji alimhukumu mwanamume huyo wa miaka 33 kifungo cha miaka 24 jela.
Mawakili wa Talluto walikuwa wametetea mteja wao wakisema vitendo vyake vilikuwa "visivyo vya busara, lakini havikuwa makusudi."
Hata hivyo, aliwaambia wale waliomwambia avalie mpira wa kondomu aliwaambia kwamba alikuwa na mzio, au kwamba muda mfupi awali alikuwa amepimwa na kupatikana hana Ukimwi, shirika la habari la AFP linasema.
Baadhi ya wanawake walipomkaripia baada ya kugundua kwamba walikuwa wameambukizwa, alikanusha madai kwamba alikuwa na virusi hivyo ambavyo husababisha Ukimwi.
Kutokana na vitendo vyake, watu wengine wanne waliambukizwa virusi hivyo kando na wanawake ambao aliwaambukiza moja kwa moja: wanaume watatu na mtoto mmoja.
Mwendesha mashtaka Elena Neri aliambia mahakama mwezi uliopita kwamba: "Vitendo vyake vilikusudiwa kupanda mauti."
Mamake Talluto alikuwa anatumia madawa ya kulevya na aliuambukizwa pia virusi vya Ukimwi.
Alifariki Talluto akiwa na miaka minne.
Mwanamume huyo aliwaambia kwamba iwapo angekuwa anawaambukiza wanawake hao virusi makusudi, badi hangelikuwa ameunga uhusiano halisi nao.
"Wengi wa wasichana hao wanawafahamu marafiki zangu na jamaa zangu," amesema.
"Wanasema kwamba nilitaka kuwaambukiza Ukimwi watu wengi zaidi. Kama hiyo ingekwua ndiyo hali, ningeenda basi kwenye baa na kushiriki ngono kiholela, singeliwaingiza katika maisha yangu."
Majaji mjini Roma walijadiliana kuhusu hukumu dhidi yake kwa zaidi ya saa 10 kabla ya kutangaza hukumu hiyo.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari Italia, mhukumiwa alilia hukumu ilipokuwa inasomwa.
Hata hivyo, adhabu hiyo haikufikia hukumu ya kufungwa jela maisha ambayo viongozi wa mashtaka walikuwa ameomba mahakama ahukumiwe.
No comments:
Post a Comment