Wednesday, October 4

Museveni mbioni kuvuka kiunzi cha mwisho cha urais wa maisha



Kinachoendelea nchini Uganda kimenikumbusha mjadala wa Waganda wawili, mmoja mfuasi wa Rais Yoweri Museveni, mwingine mfuasi wa Dk Kizza Besigye.
Anayempinga Museveni anadai kuwa kiongozi huyo ana tamaa ya madaraka huku akidai kuwa hata Idd Amin kama angeendelea kuitawala Uganda angekuwa ameshaachia madaraka muda mrefu.
Mtetezi wa Museveni anampinga kwa hoja kwamba Amin aliyetwaa madaraka kwa nguvu za kijeshi mwaka 1971 kabla ya kupinduliwa kwa msaada wa wanajeshi wa Tanzania mwaka 1979 ni dikteta, si mwanademokrasia na hafai hata kutolea mfano.
Kwa sasa nchini Uganda kuna mjadala unaoendelea kuhusu ukomo wa umri wa rais nchini humo, mjadala huu umewagawa Waganda katika makundi mawili.
Wapo wanaotaka Katiba ya nchi hiyo iheshimiwe, mwenye umri zaidi ya miaka 75 asiruhusiwe kuwa Rais na wengine wanapinga wakitaka Katiba ibadilishwe ili kusiwe na ukomo wa umri kwa mtu anayetaka kuwa Rais.
Katika mjadala huu mhusika mkuu ni Rais Museveni, kama Waganda wakisema Katiba isibadilishwe maana yake ni kwamba mwisho wa Museveni kuongoza Uganda ni mwaka 2021, kwa sasa ana miaka 73 hadi mwaka 2021 atakuwa amevuka miaka 75.
Vinginevyo Waganda wakiamua Katiba ibadilishwe na kufuta ukomo wa umri maana yake ni kwamba Museveni atakuwa na ruhusa ya kuingia katika mbio za uchaguzi mwaka 2021.
Kubadili Katiba kwa maana nyingine ni fursa ya kumfanya Museveni akiruke kiunzi pekee cha mwisho ambacho kwangu nadhani ndicho kilichokuwa kikimzuia katika safari ya kuwa Rais wa maisha wa Uganda.
Mpango wa kuitawala Uganda kwa maisha yake yote inaonekana ni azma ya muda mrefu ya Rais Museveni ambayo japo hajaitamka lakini imekuwa ikithibitishwa na kauli alizowahi kuzitoa.
Moja ya kauli ya Museveni ambayo amewahi kunukuliwa akiisema ni ile ya kuwa yeye si panya ambaye anachimba shimo halafu akitokea nyoka analikimbia shimo hilo.
Kauli hiyo maana yake ni kwamba Museveni amefanya kazi kubwa sana kuikomboa Uganda na hawezi kuiacha, kauli hiyo na nyingine nyingi ni kiashirio tosha cha Museveni kuwa rais wa maisha wa Uganda.
Huko nyuma wapinzani wa Museveni walinyamazishwa kwa hoja kwamba wakati yeye na wenzake wakihaha kuikomboa Uganda wengine walijificha na baada ya Uganda kukombolewa wanapiga kelele.
Hoja hii mara nyingi imekuwa ikitumiwa na mawaziri na wanasiasa kuwajibu wapinzani wa Museveni, “mlikuwa wapi wakati tukiwa msituni kwa ajili ya kuikomboa Uganda?”
Kauli hii ilikuwa maarufu sana miaka ya 1990 na 2000 mwanzoni lakini mabadiliko ya vizazi ni kama yameizika na sasa haionekani kuwa hoja yenye mantiki kwa kizazi cha sasa hasa kwa vijana ambao miaka ya 1980 ama walikuwa shule ya msingi au hawajazaliwa.
Ukiachana na kauli hizo, Museveni pia amekuwa akitumia demokrasia yake inayolalamikiwa sehemu mbalimbali duniani katika kuitawala Uganda milele, yaani kutumia kinachoitwa uamuzi wa umma kuhalalisha utawala wake usio na ukomo.
Kwa maana nyingine Waganda wamekuwa wakishuhudia demokrasia inavyotumika vibaya kuhalalisha urais wake wa maisha.
Tangu atwae madaraka kijeshi mwaka 1986, Museveni amekuwa akiruka viunzi vya kumzuia kuendelea kuwa Rais huku akiitumia hiyo hiyo demokrasia kuhalalisha himaya yake.
Mwaka 1996 ulifanyika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia Museveni alishinda, hiyo ni baada ya kuitumia vyema miaka 10 tangu aingie madarakani kwa kuijenga Uganda kiuchumi na kuwa mfano wa kuigwa Afrika, aliendelea kushinda tena uchaguzi mwingine wa mwaka 2001.
Baada ya kushinda 2001, Museveni aliahidi asingegombea tena kwa muhula wa tatu yaani 2006 lakini mwaka 2005, chama chake cha NRM kikampitisha kuwa mgombea urais na kuibuka mshindi tukio lililoambatana na kubadili kipengele cha katiba kilichoweka ukomo wa mihula miwili kwa nafasi ya Rais nchini Uganda.
Hoja ya Museveni wakati wote ilikuwa ni moja kwamba Waganda ndio waliomtaka na asingeweza kuwakatalia na Waganda hao hao ndio walioamua kufuta kipengele cha ukomo wa mihula miwili.
Baada ya kufuta ukomo wa mihula miwili, Museveni aliendelea kupitishwa na NRM kugombea urais mwaka 2011 na 2016 na mara zote amekuwa akishinda katika chaguzi ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwa kutokuwa huru na haki.
Hivi karibuni Museveni alihojiwa na kituo cha televisheni cha Al Jazeera, aliulizwa kwa anavyong’ang’ania madaraka, anawezaje kujihakikishia kwamba siku zijazo hatoporomoka na kuishia kuitwa dikteta badala ya mwanademokrasia.
Jibu la Museveni lilikuwa rahisi tu: “Dikteta anayechaguliwa mara tano huyo lazima atakuwa dikteta mzuri, ni dikteta wa kipekee.”
Kiunzi cha mwisho cha kumpa Museveni urais wa maisha ndicho kinachojadiliwa sasa, suala la umri, tayari tumesikia vurugu ndani ya Bunge la Uganda, wabunge wamefikia hatua ya kupigana na kuumizana hoja ikiwa ni kufuta au kutofuta kipengele cha umri wa urais.
Hoja hii ikipita ni wazi Museveni hatokuwa na cha kumzuia kuwa Rais wa maisha wa Uganda na kama ana umri mrefu anaweza kuchuana na hata kumpiku Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.
Kwa sasa naziona dalili zote za Museveni kukivuka kiunzi hicho na kuwa Rais wa maisha wa Uganda, ataitumia demokrasia yake kufanikisha azma hiyo.
Kauli yake ya mwaka 2012 aliposema anadhani baada ya miaka 75 mtu hafai kuwa kiongozi imekuwa ikiibuliwa hivi karibuni katika namna ya dhihaka.
Museveni alinukuliwa akisema kwamba hamasa ya kuongoza inashuka kwa mtu mwenye umri unaozidi miaka 75 na kwa mtu anayetaka kuwa kiongozi muwajibikaji na mwenye nguvu ni vizuri awe na umri chini ya miaka 75.
Museveni aliitoa kauli hiyo wakati akiwa na miaka 68 lakini sasa mahasimu wake wanaikumbushia naye anakuja na jibu jingine rahisi tu akisema: “Nadhani tunahitaji madaktari kuthibitisha jambo hilo.
Wakati wabunge Uganda wakisakamana na kupigana vikaoni, wananchi nao wanacharurana mitaani na kwenye mitandao ya kijamii lakini mwisho wa siku demokrasia inayowapa nafasi wengi itaamua.
Wabunge wa Museveni ni wengi na bila shaka watapitisha hoja ya kufuta ukomo wa umri, baadhi yao wameanza kusema kwamba kama anayechagua yaani mpiga kura anafanya hivyo akiwa na umri wowote kwa nini anayechaguliwa awekewe kigezo cha umri?
Kama suala hilo litahamia kwa wananchi ni wazi nguvu na ujanja ule ule au demokrasia ile ile aliyoitumia kushinda chaguzi tano na hivyo kurahisisha azma yake ya kuwa Rais wa maisha wa Uganda.     

No comments:

Post a Comment