Wednesday, October 11

Mume aingia chumba cha gesti bubu kininja, ajeruhi


Mkazi wa kijiji cha Nyansurura wilayani Serengeti, Paul Chacha (24) amejeruhiwa koromeo kutokana na kile kilichotajwa kuwa ni baada ya kufumaniwa akifanya mapenzi na mke wa mtu kwenye gesti bubu.
Katika tukio hilo mume wa mtu aliingia katika chumba cha gesti hiyo kininja akipitia darini.
Mwanamke anayedaiwa kufumaniwa akiwa na Chacha, Bhoke Simion (36) mkazi wa kijiji cha Tamukeri pia amekatwa kifundo cha mguu. Tukio hilo lilitokea Oktoba 3 na majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali Teule ya Nyerere wilayani hapa.
Katibu wa hospitali hiyo, Mbona Kazare alithibitisha kuwapokea majeruhi hao wakiwa katika hali mbaya. “Chacha alikuwa na hali mbaya, hakuwa na fahamu, damu nyingi zikivuja kwenye koromeo, kichwani, usoni, miguuni, mikono na mwanamke amekatwa kifundo cha mguu wa kushoto,” alisema.
Akisimulia mkasa huo Chacha alisema, “ni mambo ya shetani tu, tulikuwa tumelala gesti bubu ghafla mumewe aliingia ndani kupitia darini na kuanza kutushambulia, alianza na mke wake na mwisho akaja kwangu na kunikata kata ili aniue.”
Alisema kabla ya mwanamume huyo kuwashambulia alifunga milango ya kuingia na kutoka hivyo hawakupata msaada wowote kwa watu na alizinduka baada ya siku mbili akajikuta hospitalini.
Kwa upande wake Bhoke alisema, “sijui nani alimwambia mume wangu maana alikuwa ameenda msibani, tukiwa tumelala tulishangaa anaingia toka darini na panga, akanikata kifundo cha mguu, nilipiga kelele kuomba msaada lakini hakuna aliyetokea,” alisema.
Alisema mbali ya kuwashambulia alichukua Sh80,000 alizowakuta nazo na kisha kutokomea.
Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Tamukeri, Mang’era Magesa alisema mtuhumiwa hajakamatwa ingawa anaonekana kijijini hapo. Kamanda wa Polisi Wilaya ya Serengeti, Mathew Mgema alisema hana taarifa hizo na kuwa atazifuatilia.     

No comments:

Post a Comment