Mheshimiwa Rais, awali ya yote naomba nikujulishe kuwa mimi kijana wako mzima kabisa huku niliko, sina ya kiafya wala ya kisaikolojia kwasababu napiga kazi sana, na tena siku hizi nina bidii sana ya kurudi nyumbani mchana kupata mlo wa mchana. Zamani nilikuwa naponea chakula cha mchana kwenye vikao kazini. Kila kikao tulikuwa tunapewa msosi wa nguvu. Ila sasa hivi mambo mazuri, hata maji ya kunywa nabeba kwenye chupa naificha ndani ya mkoba wangu hadi ofisini.
Mheshimiwa Rais, kwa mujibu wa mila na desturi zetu za kitanzania, wasukuma ni watani zangu lakini sijui kama Rais akiwa msukuma bado naweza kumtania, maana ni mtu mkubwa sana nchini. Lakini nakumbuka juzi hapa uliwatania watani zako wahehe kuwa ungekuwa wao ungejinyonga. Basi nadhani naweza kukutania hata mimi. Nisamehe lakini kama ni utani mbaya maana unaweza kutania halafu wale jamaa wanaowahi kukasirika kabla yako wakanifanya vibaya wakati mie mtani wako.
Naomba nikuhakikishie kuwa haka kamshahara ninakopokea kwangu mie ni bonge la mshahara, sina malalamiko yoyote kabisa, ila shida ni kwamba kuna matobo mengi mno huwa kanapitia kabla ya kunifikia (najaribu kuzungumza kwa kuiga lafudhi ya watani zangu kanda ya ziwa). Tatizo ni kwamba nilipoona nateseka na nyumba za kupanga nikaamua kwenda benki kukopa, sasa nakomaje?
Hapo kuna jamaa kama tisa au kumi hivi wananikata; bodi ya mkopo wanakata, benki wanakata, LAPF wanakata, TRA wanakata, NHIF wanakata, hapa kazini napo kuna mchango wa chama cha walimu wanakata, mfuko wa mazishi wanakata, SACCOS wanakata. Duh, nabakiwa na kiasi kiduchu mwishoni. Sasa mbinde kwa mwenye nyumba, na yeye anataka mwisho wa mwaka nimpe kodi yake ya mwaka mzima, ananikamua kweli haisee.
Basi ule mwaka 2015 wakati Mzee wetu wa Msoga anashiriki sherehe ya mwisho ya Mei Mosi, sijui ilikuwa Moshi au Arusha kule, sikumbuki vizuri. Jamaa fulani wa CWT wakamwonyesha Bango linasema “May day 2015, nenda shemeji, nenda, umetuachia mshahara mkia wa mbuzi, Asante sana!!”Nadhani wale jamaa hawakujua kuwa kumbe angekuja tena Rais mwingine ambaye ni shemeji yao pia. Nadhani chama chetu kilikuwa bado hakijakaa Dodoma kuamua nani aende Magogoni.
Nilikuwa nataka kukuambia kuwa kule kwetu mbwa dili sana. Tofauti na watani zetu wahehe wanaowafanya kitoweo, kwetu mbwa huwa tunamtumia kama mlinzi na msaidizi wakati wa kuwinda. Naomba nikuambie tu kuwa sisi huwa tunawinda sana ndezi, swala, digidigi, mbawala na wanyama wengine wadogo wadogo. Ila hatuvamii mapori ya akiba.
Basi bwana, tuna usemi mmoja kule kwetu kuwa ukiona mbwa wako anabwekea kwa jirani basi ujue kwako hashibi. Au huwa tunasema kuwa ukiona mbwa yuko juu ya paa basi ujue kapandishwa na hawezi kushuka mwenyewe bali atashushwa tu na waliompandisha. Niwie radhi natumia mfano wa mbwa ambaye huwa kwenu usukumani si mnyama mzuri wa kutumiwa kama mfano. Nisamehe sana mtani.
Nilichotaka kukuambia ni kuwa Mheshimiwa Rais, nisikufiche na wala nisiwe mnafiki kwako. Mie huwa nakufagilia sana. Vijana wa mtaani huwa tunawaita wachapakazi kama wewe kuwa ni jembe. Labda nitumie lugha ya jirani zako wa kule Chato, “infwakt, huwa unanitouch sana kwa utendaji wako”. Siku ile ulipotangazwa kule Dodoma kuwa umepitishwa kuwa mgombea nilishangilia sana. Nilishakuwa na mahaba sana na utendaji wako.
Unaipenda sana nchi yako, na tumeona uchungu wako katika mambo makubwa karibia 25 tangu uingie madarakani Novemba 5 2015. Muda wote ulipokuwa ukiwanyoosha jamaa kule bandarini, TRA, NIDA, Tanesco, Bodi ya Mikopo, wizarani, nk, mie nilikuwa nashangilia sana kuwa jembe letu liko kazini. Na kwa kweli nchi ilioza kinoma. Si wewe mwenyewe umeona jinsi wale jamaa zetu walivyokuja kukupigia magoti na kukiri kuwa walikuwa wanatuibia. Nakuunga mkono sana mheshimiwa.
Ila naona kama wahenga walivyosema kwa mwenzio msiba, kwako matanga. Naona sasa imefika zamu yangu kunyooshwa. Mkwara wako wa juzi juzi hapo ulipokuwa unaongea na wale madiwani wetu pale Julius Nyerere Convention Centre ndo ukanikata maini kabisa. Lakini hata hivyo bado sijakata tamaa kuwa shabiki yako. Hata hao jamaa zako hapo kwako wanajua mie shabiki wako sana.
Ila Mheshimiwa Rais, tuhurumie basi wafanyakazi wako. Tulikuwa tunapigia sana hesabu hako kamshahara tukiamini kakiongezeka kidogo basi tupate nafuu ya maisha, walau tuhamie na sisi kwenye vijumba vyetu. Cha kuazima hakisitiri matako, tumepanga nyumba mpaka watoto wanatuonea huruma siku wenye nyumba wakija kudai kodi, huwa tunatia huruma kiasi kwamba hata wake zetu tunawaona kama mama mkwe!
Mzee, hebu fikiria mwalimu wa shule ya msingi anapokea kiduchu vile halafu na CWT wanamkata, TRA wanamkata, NHIF wanamkata, VICOBA wanamkata; ila heri yake hadaiwi na bodi ya mkopo. Jaribu kutufikiria na sisi wanaume ambao tumejaliwa kuwa wapole kama maji ya kwenye mtungi, wake zetu wakichuma hela zao hatuzigusi lakini bado wanatukaba koo kwenye hiki kidogo tunachopata.
Naogopa kunukuu ahadi zako kipindi kile cha kampeni na mwaka jana kule Dodoma kama sijakosea mzee siku ya Mei Mosi. Siku hizi sisi tunaoandika tukikosea kunukuu inakula kwetu, ila naomba tu ujue kuwa tunakutegemea sana Mheshimiwa. Ila tunaomba ujaribu kuchungulia kidogo mikoba yako tuangalizie kidogo na siye tupate ahueni kidogo. Natamani ningekuwa na uwezo siku ile ningekuomba ukaushie (kama wanavyosema vijana), tungeendelea kuishi kwa matumaini. Mzee, najua unaelewa kauli yako ndo ya mwisho nchini, ukisema wewe ndo basi tena.
Kama sijakosea, chama chetu cha Mapinduzi kina nembo ya Jembe na Nyundo kumaanisha jembe ni wakulima na nyundo ni wafanyakazi. Hawa wote ni watu wa chini sana katika taifa hili na ni matabaka yanayonyonywa sana. Bado siamini kama ulikuwa “serious” siku ile, unajua tatizo watu hawajui kutofautisha unapotania na unapokuwa serious. Kuchomekea utani ni kawaida kabisa.
Tusaidie walau na siye tujisikie tunafurahia kuwa watumishi wa Serikali ya Tanzania. Sitaki kabisa nione walimu, wauguzi, askari na wafanyakazi wengine wadogo walioko vijijini wakifanya kampeni mbaya mwaka 2020. Ila ukiwanyima hawa jamaa wenye magari, posho, ruzuku, na nyumba haina shida kabisa, wao wanachopokea kinatosha kutunzia watoto. Cha msingi wapunguze tu kupitia UDASA kila jioni. Asante sana Mheshimiwa Rais.
0787525396
No comments:
Post a Comment