Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Sensa ya Watu na Takwimu za Jamii, Ephraim Kwesigabo alisema ongezeko hilo limechangiwa na kupanda kwa bei za vyakula na nyinginezo.
“Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia ongezeko hilo ni dagaa asilimia 7.6, matunda makavu kama nazi kwa (3.1), viazi vitamu kwa (3.0), mchele (1.5) na ndizi (1.5),” alisema Kwesigabo. Bidhaa nyingine zilizochangia ni mkaa kwa asilimia 4.0, dizeli (2.4) na petroli (0.6).
“Farihisi za nishati na mafuta, vyakula na vinywaji baridi zimekuwa na mwenendo wa juu kwa kipindi chote zikilinganishwa na farihisi nyingine,” alisema Kwesigabo.
Alisema kundi la nishati na mafuta limekuwa na mwenendo usio imara ikilinganishwa na makundi mengine kwa kipindi husika, huku bidhaa zisizojumuisha chakula zikionyesha mwenendo wa bei ulio imara.
Pia, Kwesigabo alisema mfumuko wa bei za vyakula vya nyumbani na migahawani umeongezeka hadi asilimia 9.8 kwa Septemba kutoka asilimia 9.1 Agosti, huku mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa Septemba ukipungua hadi asilimia 1.7 kutoka 1.8 ya Agosti.
Naye Meneja wa Takwimu za Ajira na Bei, Ruth Minja alisema uwezo wa Shilingi ya Tanzania kununua bidhaa na huduma umefikia Sh92.18 kwa Septemba ikilinganishwa na Sh92.20 ya Agosti.
No comments:
Post a Comment