Mwishoni mwa wiki, Rais Magufuli alifanya mabadiliko ya baraza lake la mawaziri ikiwa ni pamoja na kuongeza wizara mbili.
Mawaziri walioapishwa jana na wizara zao ni Angela Kairuki (Madini), Dk Charles Tizeba (Kilimo), George Mkuchika (Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma), Luhaga Mpina (Mifugo na Uvuvi) na Dk Hamis Kigwangallah (Maliasili na Utalii).
Wengine ni Selemani Jafo (Ofisi ya Rais - Tamisemi), Dk Medard Kalemani (Nishati) na Isaac Kamwelwe (Maji na Umwagiliaji).
Manaibu waziri ni Stella Manyanya (Viwanda, Biashara na Uwekezaji), William Ole Nasha (Elimu, Sayansi na Teknolojia), Josephat Kandege (Tamisemi), Kangi Lugola (OMR – Muungano na Mazingira), Dk Faustine Ndugulile (Afya) na Subira Mgalu (Nishati).
Wengine ni Mary Mwanjelwa (Kilimo), Atashasta Nditiye (Uchukuzi na Mawasiliano), Japhet Hasunga (Maliasili na Utalii), Abdallah Ulega (Mifugo na Uvuvi), Stanslaus Nyongo (Madini), Elias Kwandikwa (Ujenzi), Joseph Kakunda (Tamisemi), Stella Ikupa (OWM – Wenye Ulemavu), Juma Aweso (Maji na Umwagiliaji) na Juliana Shonza (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo).
Wakizungumza baada ya kuapishwa, baadhi ya mawaziri hao walimshukuru Rais Magufuli kwa kuwaamini na kuwapa majukumu ya kulitumikia Taifa huku wakiahidi kwamba wamejipanga kwenda kukabiliana na changamoto zinazolikabili Taifa.
Akizungumzia mikakati yake, Dk Kigwangallah alisema mojawapo ni kumaliza mgogoro wa Loliondo; kupambana na ujangili na kubuni mbinu za kutangaza vivutio vya utalii duniani kote.
Dk Kigwangallah alisema wizara yake itafanya sensa ya vivutio vya utalii nchi nzima na kuweka mikakakti ya kuvitangaza kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwatumia wasanii wa ndani na nje ya nchi.
“Sasa kuna soko kubwa la watalii kutoka China, lazima tuangalie namna ya kutangaza vivutio vyetu katika ukanda huo. Utalii unachangia asilimia 25 ya fedha za kigeni hapa nchini, tunaweza kufanya vizuri zaidi ya hapo,” alisema Dk Kigwangallah.
Alipoulizwa kuhusu mfululizo wa mawaziri kuondolewa katika wizara hiyo, Dk Kigwangallah alisema ili kubaki salama katika wizara hiyo lazima kuwa na uhusiano mzuri na wananchi na uadilifu katika kazi.
“Natambua ni wizara ngumu ambayo inahitaji umakini mkubwa. Namshukuru Rais Magufuli kwa kuniamini na kunipa jukumu kubwa, nimejipanga kufanya kazi kwa ubunifu,” alisema Dk Kigwangallah ambaye alikuwa naibu waziri wa afya, ustawi wa jamii, wazee na watoto.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Angela Kairuki alisema anatambua kwamba madini ni injini ya uchumi wa nchi, kwa hiyo ataangalia namna ya kuifanya sekta hiyo inalinufaisha taifa kwa kuwaletea wananchi maendeleo.
Kairuki alisema wataangalia changamoto katika sekta hiyo na kuweka mikakati. Waziri huyo alisema watakwenda kufanya maboresho ya sheria na kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Tunaingia kwenye hii wizara tukiwa na mawazo chanya tukiamini kuwa wapo wataalamu wa kutosha ambao tutafanya nao kazi. Hali ya uwekezaji ni shwari na imekuwa ndiyo sera ya serikali yetu,” alisema Kairuki ambaye anakuwa mwanamke wa kwanza kuongoza wizara hiyo mpya.
Akizungumzia historia ya sekta hiyo kuwang’oa mawaziri, Kairuki alisema “ngoja niende, sijawahi kukaa kwenye madini, nikifika huko nitajua nini cha kufanya. Ni ngumu kujua kwa sasa.”
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika alisema anakwenda kuangalia stahiki za wafanyakazi na kupambana na rushwa nchini.
Mkuchika alisema atawasiliana na waziri wa elimu kuangalia uwezekano wa kuweka somo la rushwa kwenye mtaala ili watoto wajifunze ubaya wa rushwa wakiwa bado wadogo na kukua katika maadili.
“Nitaongea na waziri wa elimu ili somo linalohusu rushwa linafundishwa kuanzia shule za msingi,” alisema Mkuchika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tamisemi, Seleman Jafo aliwataka watendaji wa Serikali kujipanga kufanya kazi na kwamba atasimamia nidhamu ya utendaji kazi ili kupata matokeo yanayokusudiwa.
Jafo amewataka wakurugenzi, wakuu wa wilaya na mikoa kusimamia vizuri utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kuzingatia nidhamu na sheria za nchi na zile za maeneo yao.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alisema sekta za mifugo na uvuvi ni kuhimu sana kwa uchumi wa taifa lakini kwa bahati mbaya serikali imekuwa hainufaiki na sekta hiyo licha ya umuhimu wake.
“Manufaa ambayo taifa limepata kutokana na sekta hizo ni kidogo sana, kwa hiyo ninakwenda kushirikiana na wenzangu kuona ni jinsi gani mifugo inapata masoko, viwanda vya kusindika nyama vinaanzishwa na uvuvi wa kitaalamu unafanyika,” alisema Mpina ambaye alikuwa Naibu Waziri OMR – Muungano na Mazingira.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais - Muungano na Mazingira, Kangi Lugola alisema uwaziri aliopewa ni mdomo wake wa pili na sasa anakwenda kutekeleza yote ambayo amekuwa akiikosoa Serikali.
“Mdogo wangu hautafungwa, nitakwenda kushughulika na wale wote wanaofanya watu wakose chakula, wakose maji safi. Tunakwenda kuwafanya waziheshimu sheria za nchi,” alisema Lugola ambaye amepata umaarufu kwa kuikosoa Serikali.
Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alisema anakwenda kufanya kazi kwa kufuata Katiba ya nchi, sheria na kanuni za Bunge.
No comments:
Post a Comment