Siku kadhaa zilizopita Rais John Magufuli amefanya mabadiliko ya baraza la mawaziri kwa kuchagua mawaziri wapya na kuongeza idadi ya wizara.
Mawaziri wameongezeka kutoka 19 hadi 21, mawaziri wapya 14 wameteuliwa, wanne wameachwa huku naibu mawaziri wanne wakipandishwa vyeo na kuwa mawaziri kamili.
Alilazimika kufanya mabadiliko hayo baada ya kutengua uteuzi wa waziri wa zamani wa nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo na kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene na Naibu Waziri wa Ujenzi, Edwin Ngonyani.
Wizara ya Nishati na Madini sasa imetenganishwa na kuwa wizara mbili tofauti pia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nayo imegawanywa na kuwa wizara mbili.
Mabadiliko hayo yanatafsiriliwa kama ni kujipanga upya kwa Serikali, pia kuna waliosifu kwamba yataongeza ufanisi wa kazi katika wizara huku wengine wakikosoa kuwa Rais ameenda kinyume na ahadi yake ya kuwa na baraza dogo kama njia ya kubana matumizi.
Hiyo ilikuwa ni dondoo tu kuhusiana na mabadiliko ya Serikali ya Awamu ya Tano, lakini lengo langu sio kuzungumzia uundwaji wa baraza hilo bali utendaji wa wateule wapya katika kuziongoza wizara hizo kwa maendeleo ya nchi.
Wizara kama ya Madini na Nishati ambazo awali zilikuwa zimeungana ni wizara nyeti ambazo wengi waliopita waliondoka na kashfa na huenda hawakuzingatia weledi.
Wizara zote mbili zinaaminika kuwa na ushawishi mkubwa wa rushwa, kutokana na wadau wake kutumia fedha nyingi kwa masilahi binafsi na uhitaji wa rasilimali zinazosimamiwa kuwa dili.
Lakini, kama asemavyo Rais Magufuli kila wakati, kazi ya utumishi wa umma sio ya kufurahia kwamba unakwenda kuvuna pesa, bali kutanguliza uzalendo na masilahi ya Taifa kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Mawaziri wanalipwa mishahara mizuri, wanapewa magari ya kutembelea na huduma nyingine muhimu ili kuwaepusha na changamoto mbalimbali, lakini pia tamaa ya rushwa na matendo mengine yaliyo kinyume na kiapo chao.
Mawaziri na watumishi wengine wa umma wanapaswa kuishi katika viapo vyao, kufuata kanuni za utumishi na utawala bora, sheria na Katiba bila kusahau kufanya kazi katika mipaka yao.
Utulivu wa fikra kabla ya maamuzi unasaidia kutambua ni jambo gani au hatua gani sahihi inapaswa kuchukuliwa kuhusiana na jambo fulani. Rejea za wapi watangulizi walijikwaa na wapi walisimama imara ni mambo mhimu pia ambayo mawaziri hao wa sasa wanapaswa kuangalia.
Katika kila jambo la nchi masilahi ya Taifa yanapaswa kutangulia kwanza, kabla ya masilahi binafsi ili kuweza kulisukuma gurudumu la maendeleo katika ya nyanja zote.
Ni mhimu kila waziri kwa nafasi yake akijua dira ya maendeleo ya nchi, lakini pia kuweka kando siasa kwenye masuala ya kiutendaji na kuweka siasa mahali panapohitaji siasa.
Siasa kwenye masuala yasiyohitaji siasa kama ya kiutendaji ni kikwazo kikubwa katika kuyafanikisha yaliokusudiwa, kwani utaalamu utakuwa unapingwa na wasio wataalamu.
Hata hivyo, kila waziri anapaswa kukumbuka kuwa anayo nafasi ya kumshauri Rais katika mfumo rasmi uliowekwa na kumsaidia kusukuma maendeleo ya sekta zilizopo chini ya wizara yake kwa masilahi ya Taifa zima.
Bila woga na kwa namna inayofaa, kila waziri anapaswa kumshauri kiongozi mkuu wa nchi katika masuala yenye tija kwa Watanzania kwani Rais hawezi kujua na kufanya mambo yote pekee yake.
Aidha, mawaziri hawapaswi kulewa madaraka kama walivyofanya waliowahi kufanya kwani madhara yake ni makubwa katika utendaji, uongozi na kuwahudumia wananchi.
Kila mmoja awajibike na amuwajibishe anayepaswa kumuwajibisha kwa mujibu wa sheria na taratibu bila uonevu, chuki wala visasi.
Ni rahisi watendaji walio chini kuiga mfumo mzuri wa utumishi wa umma, endapo wasimamizi wao watakuwa mfano kuigwa.
Ushirikiano baina ya waziri na watumishi walio chini yake una nafasi kubwa ya kufanikisha mipango ya kitaifa iliyopo katika wizara husika.
Nchi yetu bado inaendelea, hivyo inahitaji viongozi wachapa kazi na wenye uwezo wa kuthubutu katika kuchukua hatua zinazolenga kuleta maendeleo katika nyaja zote muhimu za maisha.
Ulinzi wa rasilimali za nchi na kupigania ukuaji wa uchumi katika Taifa unapaswa kuwa wajibu wa kila mmoja.
Wananchi nao wanapaswa kuendelea kuwapa ushirikiano viongozi wa Serikali yao ili waweze kutimiza majukumu yao ipasavyo na baadaye Tanzania iweze kusonga mbele kimaendeleo.
Ephrahim Bahemu
ephraimbahemu@gmail.vom
0756939401
No comments:
Post a Comment