Tuesday, October 10

MADAKTARI BINGWA 18 KUTOKA SAUDI ARABIA KUWASILI ZANZIBAR


Kundi la madaktari bingwa 18 wa hiyari kutoka nchini Saudi Arabia linatarajiwa kuwasili tarehe 12 Oktoba ambapo wataweka kambi ya tiba (medical camp) kwa muda wa majuma miwili. Madaktari hao wanatarajiwa kufanya matibabu na upasuaji katika hospitali za kisiwa cha Pemba.

Akizungumza katika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania mjini Riyadh wakati wa hafla ya kuagana na madaktari hao, Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Hemedi Mgaza, alisema kambi tiba hii ni ya pili kufanyika Zanzibar. Mwezi Novemba mwaka 2016 madaktari hao walifika Zanzibar na kuweka kambi ya kwanza katika kisiwa cha Pemba kwa mara ya kwanza kwa mafanikio makubwa.

Mwaka jana madaktari hao walipata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa viongozi wa Wizara ya Afya ya Zanzibar na madaktari wenyeji, ndio maana wamependelea kurejea tena mwaka huu.

Pamoja na kutoa huduma za matibabu, madaktari hao watakwenda na dawa na vifaa tiba vya aina mbalimbali ambavyo Mwisho wa kambi watavitoa kama msaada kwenye hospitali hizo.
Katika picha ni viongozi wa Madaktari wakiwa na Balozi Hemedi Mgaza na Afisa wa Ubalozi Bw. Ahmada Sufiani walipofika Ubalozi mjini Riyadh kujitambulisha.

No comments:

Post a Comment