Watu 2,183,629 waliojiandikisha kupiga kura watafika vituoni kesho kumchagua rais mpya ambaye atarithi kiti cha Rais Ellen Johnson Sirleaf anayestaafu baada ya kuongoza vipindi viwili vya miaka sita kila kimoja.
Milango katika vituo vya uchaguzi itafunguliwa saa 2.00 asubuhi na itafungwa saa 12.00 jioni. Katika uchaguzi huo wa baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, mbali ya kumchagua rais pia watawachagua wawakilishi 73 wa Bunge.
Uchaguzi huo unatarajiwa kuwa wa kwanza wa kidemokrasia kwa rais kukabidhi kiti kwa mwingine tangu ilipofanyika hivyo mwaka 1943 wakati William Tubman alipochaguliwa kwa amani kumrithi Edwin Barclay
Huu utakuwa uchaguzi wa tatu tangu mwaka 2003, baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe. Rais wa kwanza mwanamke Ellen Johnson Sirleaf, aliyejitahisi kusimamia amani na utulivu anastaafu huku nafasi yake ikigombaniwa na wanasiasa 20 wakiwemo nyota wa zamani wa soka George Weah na mgombea pekee wa kike MacDella Cooper.
Ellen ameweka historia kuwa mwanamke wa kwanza kuongoza barani Afrika na wa kwanza kuachia ngazi.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), waliojiandikisha ni wanawake 1,064,274 sawa na asilimia 41 na waliosalia yaani 1,119,355 sawa na asilimia 51 ni wanaume.
Kampeni za mwisho zilifanywa juzi. Lakini licha ya umati mkubwa wa watu ambao umekuwa ukihudhuria katika kampeni za wagombea hali iliyosababisha asasi za maoni “kuwapa alama nyingi baadhi ya wagombea” baadhi ya wadadisi wa masuala ya siasa wamekumbuka maneno ya Rais Donald Trump wa Marekani.
Trump katika kampeni hizo alisema kwamba atamshinda mpinzani wake Hillary Clinton na kuwathibitishia wapigakura za maoni kuwa waongo kwa sababu “harakati” zake zilikuwa zinakwenda vizuri. Trump alimshinda Hillary ambaye alikuwa akipewa nafasi kubwa na wachambuzi wa siasa za Marekani.
Vyama vinavyopewa nafasi kubwa ya kushinda ni Unity Party (UP) ambacho mgombea wake ni Makamu wa Rais Joseph Nyuma Boakai; Congress for Democratic Change (CDC) cha Seneta George Weah, Alternative National Congress (ANC) na Liberty Party (LP) ambacho mgombea wake ni Cllr. Charles Walker Brumskine na All Liberia Party (ALP) cha mfanyabiashara Benoni Urey.
No comments:
Post a Comment