Tuesday, October 24

Kenyatta amwambia Chebukati katu hatabadilisha msimamo

Mwenyekiti wa tume ya IEBC, Wafula Chebukati, asalimiana na rais Uhuru Kenyatta baada ya wawili hao kukutana mjini Nairobi siku ya Jumatatu tarehe 23 mwezi Oktoba, 2017.
Rais Uhuru Kenyatta hatimaye amefanya mkutano na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya, Wafula Chebukati, siku mbili tu kabla ya uchaguzi wa marudio uliozua utata kufanyika nchini humo.
Kenyatta amekuwa akishinikizwa na baadhi ya wadau kukutana na afisa huyo pamoja na aliyekuwa mgombea wa urais kwa tikiti ya muungano wa NASA, Raila Odinga, ili kutatua mzozo wa kisiasa unaoendelea kuikabili nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo ulifanyika Jumatatu alasiri katika afisi ya Rais Kenyatta kwenye jengo la Harambee House jijini Nairobi.
Punde tu baada ya mkutano huo, Kenyatta alituma taarifa kwa vyombo vya habari iliyosema kuwa alimweleza mwenyekiti huyo kwamba hana masharti yoyote kwa tume hiyo, isipokwa tu kwamba uchaguzi ufanyike siku ya Alhamisi kama ilivyoagizwa na mahakama ya juu.
"Msimamo wangu ni ule ule, Wakenya wapewe nafasi ya kushiriki kwenye zoezi la kidemokrasia la kupiga kura kama tu ilivyoagizwa na mahakama ya juu. Hatuna masharti yoyote kwa IEBC," alisema Kenyatta.
Haya yliijiri huku takriban mabalozi wanaowakilisha nchi zao mjini Nairobi wakitoa shinikizo kwa wadau wote kutochukua hatua ambazo huenda zikachangia kuzorota kwa hali ya usalama.
"Ni rahisi kubomoa kuliko kujenga," alisema Robert Godec, balozi wa Marekani nchini Kenya, ambaye alisoma taarifa hiyo ya pamoja mjini Nairobi.
Godec alionya dhidi ya mashambulizi yanayolenga maafisa wa tume ya IEBC na kuongeza kuwa iwapo tume hiyo imebaini kwamba haitaweza kusimamia uchaguzi wa haki na ukweli, basi ni vyema iulize mahakama ya juu iuongeze muda wa zoezi hilo ili kuepusha taharuki yoyote.
Kiongozi wa muungano wa NASA naye aliendelea na mikutano ya hadhara katika kaunti ya Kisii na kuwataka wafuasi wake kutoshiriki kwenye uchaguzi huo wa Alhamisi.
"Oktoba hakuna uchaguzi," alisema mwanasiasa huyo.

No comments:

Post a Comment