Tuesday, October 24

Kenya yagawika ikielekea uchaguzi mpya wa Rais Okt 26

Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika zimetoa wito wa kuwepo amani nchini Kenya huku hali ya wasiwasi nchini humo ikizidi kabla ya uchaguzi wa Alhamisi wiki hii.

Kenia Päsident Kenyatta (Reuters/B. Ratner)
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais  wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat wamesema pande mbili za kisiasa Kenya zinapaswa kujizuia dhidi ya kuchochea ghasia na kuvitaka vikosi vya usalama vya Kenya pia kujizuia dhidi ya kutumia nguvu kupita kiasi.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis pia ametoa wito wa kuwepo mazungumzo ya tija Kenya ambako anasema anafuatilia kwa karibu yanayojiri nchini humo na kuongeza analiombea taifa la Kenya liweze kukabiliana na changamoto linalozikabili katika mazingira ya majadiliano ya tija yaliyo na lengo la kufikia mazuri.
Wito wa amani watolewa kabla ya uchaguzi
Akiliongoza taifa katika maombi kwa ajili ya amani hapo jana, Rais Uhuru Kenyatta amewaomba wakenya kudumisha amani kabla ya uchaguzi wa Alhamisi.
Kenia Raila Odinga bei Kundgebung in Mombasa (Reuters/J. Okanga)
Kiongozi wa upinzani Raila Odinga
Wakati huo huo, Waendesha mashitaka watamshitaki dada yake Odinga, Ruth Odinga, seneta wa kaunti ya Kisumu Fred Outa  pamoja na watu wengine kwa kuchochea ghasia baada ya maafisa wa tume ya uchaguzi kushambuliwa wiki iliyopita mjini Kisumu. Mashitaka mengine dhidi yao ni uharibifu wa mali, kuwazuia maafisa wa uchaguzi kuendesha shughuli zao na kukivamia kituo cha tume hiyo.
 Maandamano ya karibu kila siku wakati mwingine yakiwa ya vurugu, cheche za maneno kutoka kwa wanasiasa na hali ya sintofahamu iliyoko Kenya kabla ya uchaguzi mpya wa rais unaotarajiwa Alhamisi wiki hii umeiweka nchi hiyo katika hali ya mashaka na kugawika.
Maandamano ya umma yamekuwa tukio la karibu kila siku tangu uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika Agosti nane kufutiliwa mbali na mahakama ya juu. Uchaguzi huo ulikuwa umempa ushindi Rais Uhuru Kenyatta dhidi ya mpinzani wake Raila Odinga.
Uhasama ulioongezeka unatia wasiwasi
Waandamanaji wamekuwa wakirushiwa gesi ya kutoa machozi, wanasiasa wa upinzani kukamatwa na wiki iliyopita kamishna mmoja wa tume ya uchaguzi IEBC Roselyn Akombe alitorokea Marekani akihofia maisha yake na kudai kuwa hakuna vile uchaguzi wa Oktoba 26 utakuwa wa huru na wa haki.
Kenia Proteste in Nairobi (Reuters/T. Mukoya)
Waandamanaji wakirushiwa gesi ya kutoa machozi mjini Nairobi
Badala ya uchaguzi huo mpya kutuliza hali nchini Kenya, unaonekana kuleta hali ya taharuki. Odinga, kiongozi wa muungano wa Nasa ameitisha maandamano siku hiyo ya uchaguzi baada ya mapema mwezi huu kutangaza hatashiriki katika uchaguzi huo kwasababu matakwa yake ya kuwepo mageuzi katika tume ya uchaguzi hayakutimizwa.
Kwa upande wake, Rais Uhuru Kenyatta ambaye aliuita uamuzi wa mahakama wa kuufutilia mbali uchaguzi wa rais wa Agosti nane kuwa ni 'mapinduzi', ameapa kushiriki katika uchaguzi wa Alhamisi hata kama mpinzani wake hatashiriki, hatua ambayo wachambuzi wanasema itaufanya uchaguzi huo mpya kutotambulika kisheria.
Jared Jeffrey mchambuzi wa shirika la kutoa ushauri wa kiuchumi barani Afrika NKC anaashiria  kuwa Kenya huenda ikatumbukia katika ghasia iwapo uchaguzi huo utaendelea akiongeza kuwa upande wa Odinga huenda ukaanzisha wimbi jipya la maandamano zaidi.

No comments:

Post a Comment