Lugola ni miongoni mwa wabunge wa chama tawala ambaye alikuwa akitekeleza wajibu wake wa kuibana Serikali na wakati mwingine akitumia mavazi na vifaa visivyotakiwa ndani ya Bunge kuonyesha msisitizo wa hoja zake.
Amewahi kuvaa ‘maski’ mithili ya ninja, kuingia bungeni na sare ya CCM, kubeba nyembe mdomoni ili kwenda kuionyesha Serikali ilivyoshindwa kuwa na kiwanda hata cha kuzitengeneza na vijiti vinavyotumika kutoa mabaki ya chakula kwenye meno.
Kwa kuwa sasa atakuwa upande mwingine wa Serikali, swali lililopo ni kwa namna gani atatekeleza kile alichokuwa akikipigania bungeni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi?
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Keissy akizungumzia hilo jana alisema, “Si unajua waziri bungeni hachangii… itabidi azungumze katika Baraza la Mawaziri sasa. Kwa kuwa ameingia jikoni akayafanye yale aliyokuwa anayasema na mimi ninaona ataweza kuyafanya.”
Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bungara maarufu Bwege alisema, “Kwa uzoefu wetu, mtu akiwa mbunge akiteuliwa tu kuwa waziri au naibu waziri anakuwa kazibwa mdomo. Ujue yeye ndiye atakuwa akiulizwa maswali sasa lazima aitetee Serikali.”
Lugola hakupatikana jana kuzungumzia uteuzi wake.
Wakati wa mjadala wa sakata la ufisadi wa uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow Novemba 28, 2014 Lugola aliamua kuvaa kofia maarufu ‘maski’ akieleza kwamba kufanya hivyo kutamwezesha kusema ukweli na kutomwonea haya mtu.
“Mheshimiwa mwenyekiti (Azzan Zungu) kama kanuni zinaruhusu naomba uniruhusu nichangie hoja hii nikiwa nimevaa kininja ili nisiwatazame usoni,” alisema Lugola huku akichukua kofia na kuivaa. Hata hivyo, Zungu alimtaka aivue kwa kuwa kanuni za Bunge haziruhusu.
“Mheshimiwa mwenyekiti, mimi ni mbunge wa CCM, ahadi namba nane ya mwana CCM inasema; nitasema kweli daima fitina kwangu mwiko na ibara ya tano inaonyesha malengo na dhumuni la CCM, nimepitia malengo yote hakuna ambapo inasema CCM itatetea wezi.”
Katika kujenga hoja yake Lugola hakuishia hapo, aliomba avae mavazi ya CCM ili kutekeleza ahadi namba nane. Alichukua shati la kijani na kofia jambo ambalo Zungu alilipinga, huku wabunge wakishangilia.
Juni 10, 2016 alikuwa miongoni mwa wabunge wa CCM aliyesimama kidete kupinga pendekezo la Serikali la kukata mapato ya viinua mgongo vya wabunge akimtaka Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kutowachezea wabunge.
Pia, amewahi kwenda na kile alichokiita kontena la bidhaa akieleza ameliacha nje na kwamba ndani ya Bunge ameingia na baadhi ya bidhaa hizo ukiwamo wembe aliouficha mdomoni ili mashine za ukaguzi zisimbaini lengo likiwa ni kuionyesha Serikali ilivyoshindwa hata kuwa na kiwanda cha bidhaa ndogondogo.
Mei 12, akichangia bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka wa fedha wa 2017/18, aliwahamasisha wabunge kutoipitisha kama haitakuwa na mwarobaini wa tatizo la huduma za maji nchini.
Lugola alisema wabunge watakaoipitisha atazikusanya sauti zao za ndiyo na kuzunguka nazo nchi nzima kwenda kuwashtaki kwa wananchi kwa kitendo chao cha kuwasaliti.
No comments:
Post a Comment