Dar es Salaam. Waziri mkuu wa zamani, Jaji mstaafu Joseph Warioba amewataka viongozi kujenga utamaduni wa kukutana wanapogundua kuna matukio yanayoashiria uvunjifu wa amani na kuzungumzia kwa umoja kama wafanyavyo viongozi wa dini.
Jaji Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba alisema licha ya kuwapo viashiria vya kuvunjika kwa amani, tatizo kubwa linaloonekana ni viongozi hasa wanasiasa kuogopa kuzungumzia matatizo yanayolikabili Taifa.
Akifungua mdahalo wa mashauriano juu ya kuhamasisha, kusisitiza, kulinda na kudumisha amani, umoja na maridhiano nchini ulioandaliwa na taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation (MNF), Jaji Warioba alisema waasisi wa Taifa walijenga umoja na misingi ya maendeleo ambayo kuna dalili ya kutoweka.
Alisema viongozi wa dini wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kunusuru amani iliyopo kwa kukutana mara kwa mara bila kujali imani zao pale wanapoona mambo hayaendi sawa.
“Tatizo ninaloliona ni kwamba tunaogopa kuzungumzia matatizo yetu. Niwashukuru viongozi wa dini wamekuwa wepesi mno kukutana na kuzungumza pale wanapoona kuna viashiria vya uvunjifu wa amani. Kutokana na hilo naweza kusema viongozi wa dini wana mchango mkubwa katika kuinusuru amani ambayo tunayo sasa,” alisema.
Jaji Warioba alisema kuna viashiria vya kutoweka kwa amani na viongozi wa kiserikali na kisiasa wanapaswa kuiga kile wanachofanya wenzao wa dini. “Amani ikitoweka kuirudisha ni ngumu mno. Viongozi hasa hawa wa kisiasa wawe wepesi kukutana na kuzungumza. Tuache malumbano hasa viongozi wa kisiasa na tukiendelea wanaweza kutufikisha pabaya,” alisema Jaji Warioba. Alisema kila Mtanzania ana jukumu la kushiriki katika ulinzi wa Taifa na kuhakikisha amani inaendelea kuwapo. Kuhusu mtindo wa wanasiasa kutumia vyombo vya habari alisema: “Hata kama wanatumia mitandao ya kijamii au vyombo vya habari kujibizana, ni muhimu wawe tayari kukutana kama wanavyofanya viongozi wa dini na kujadiliana kwa masilahi ya Taifa.”
“Nchi haiwezi kuendeshwa kwa huyu kuongea hiki, huyu naye anamjibu kupitia vyombo vya habari. Hapana, hawa watu wakae wazungumze.”
Kuhusu mdahalo huo, msaidizi maalumu wa mkurugenzi mtendaji wa MNF, Gallus Abeid alisema umefanyika wakati muafaka hasa baada ya kuona uwepo wa dalili za uvunjifu wa amani.
Alisema: “Tumeona ni vizuri tufanye sasa kwa sababu zipo dalili zinazoashiria tunda hili la amani linapata dosari, kama mnavyoona hali ya nchi yetu katika siku za hivi karibuni. Kuna vitu tunapaswa kuvishughulikia ili kuimarisha amani na umoja.”
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Ernest Kadiva alisema hata Mungu alimshusha mwanae kuja kuzungumza nasi na kwamba mazungumzo ni jambo kubwa na lenye tija. “Kukaa na kuzungumza ni muhimu kwa kuwa kila mtu anakuwa na upeo wake, wanapokutana chumbani na kuzungumza, watapingana kwa hoja, watatofautiana na watakapokuja huku nje wanakuwa kitu kimoja ili kuepuka kuwagawa wananchi,” alisema Mchungaji Kadavi.
Alisema nyakati hizi ni tofauti na kipindi cha nchi ikiwa katika mfumo wa chama kimoja na kuruhusu mfumo wa vyama vingi ni lazima viongozi wakafahamu umuhimu wa kukutana na kuzungumza.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum aliunga mkono kauli ya Jaji Warioba akisema ameitoa wakati mwafaka na inapaswa kufanyiwa kazi huku akiwasihi viongozi wa kisiasa kuiga mfano wa kamati za amani kuzungumza.
“Wanasiasa wakutane na wasiogope. Hakuna haja ya kuogopana kwani wanajuana na ni jambo jema kila wanapokutana na kuzungumza kwani hakuna mwenye hatimiliki na Taifa, hivyo wakutane na wazungumze,” alisema Sheikh Salum.
“Wote ni Watanzania, kukosoana ndio ubinadamu na hakuna binadamu aliyekamilika, Tanzania ya amani inapaswa kuendelea,” aliongeza.
Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia alisema taifa lolote duniani haliwezi kuendelea pasi na kuwa na meza ya majadiliano kwa mambo mbalimbali yenye manufaa kwao.
“Jaji Warioba amezungumza umuhimu wa kukutana na hata Mwalimu Nyerere alisisitiza amani, umoja na maendeleo kwa kuzingatia majadiliano, lakini sasa hatuoni majadiliano hayo yakifanyika,” alisema Mbatia.
“Ni wakati sasa kwa wanachama wa TCD, vyama vyenye wawakilishi ndani ya Bunge vya CCM, Chadema, NCCR-Mageuzi, CUF na ACT-Wazalendo wakutane na kuzungumza changamoto tunazokutana nazo na kuzitafutia ufumbuzi,” aliongeza.
No comments:
Post a Comment