Saturday, October 28

Familia yaelezea ilivyopoteza ndugu kutokana na mvua

Wakazi wa Kilvya wakibeba mwili marehemu, Issa
Wakazi wa Kilvya wakibeba mwili marehemu, Issa Ali aliyekuwa askati wa Suma JKT ambaye ni mmoja wa wati sita wanaodaiwa kufa maji katika mto Mpakani uliyop Kiluvya, Dar es Salaam. Picha na Said Khamis  
Dar es Salaam. Kuna usemi kuwa mvua inaponyesha huleta neema na hufurahiwa zaidi na wakulima kwa sababu ni dalili ya kuwapo kwa mavuno mengi msimu huo.
Lakini, hali haikuwa hivyo kwa baadhi ya familia ambazo zilijikuta zikipata balaa na majanga.
Familia ya Nolasco Mashele haiwezi kuwa na furaha hata kidogo kutokana na mvua hizo za siku mbili mfululizo zilizonyesha jijini hapa.
Familia hiyo imempoteza mtoto wao, Theresia Mashele (8) na jirani yao Issa Ally (28) aliyekuwa mfanyakazi wa Suma JKT aliyefariki wakati akijaribu kumuokoa mtoto huyo.
Mvua hiyo, ambayo ilinyesha Jumatano na Alhamisi ilisababisha nyumba kadhaa kubomoka na watu wanne kupoteza maisha huku kaya zaidi ya 20 za maeneo ya Kiluvya zikikosa makazi baada ya nyumba zao kuingiliwa na maji na nyingine kubomoka.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa alisema mvua hiyo ilisababisha watu wanne kufariki dunia akiwamo Issa na Theresia, huku miundombinu ya barabara na madaraja yakiharibika pia.
Kifo cha Theresia
Wakati mvua ikiendelea kunyesha juzi nyumba ya familia ya Mashele iliingiliwa na maji huku watoto watatu wakiwa ndani pamoja na dada yao jambo ambalo liliwafanya wapige kelele kuomba msaada wa majirani.
Akielezea tukio hilo baba wa marehemu, Nolasco Mashele alisema asubuhi wakati anaondoka kwenda kazini aliwaambia watoto wake wasiende shule kwa sababu mvua ilikuwa kubwa. Watoto walitii agizo hilo.
Wakiwa nyumbani mvua iliendelea kunyesha hadi ilipofika saa nne asubuhi maji yalipoanza kuingia ndani ya nyumba hiyo baada ya kuacha njia yake.
“Tukio hilo likawashtua wanangu na kuanza kupiga kelele wakiomba msaada kwa majirani,” anasimulia Mashele.
“Majirani walifika na kuanza kuwaokoa watoto hao. Mmoja wa majirani waliofika ni Issa Ally (marehemu) na Joseph Mbwela aliyenusurika,”
“Majirani hao waliingia katika nyumba hiyo wakiwa na ngazi ya mbao ambayo waliisimamisha katika nyumba hiyo na kuiegesha upande wa nyumba ya jirani yao kwa lengo la kuwavusha watoto hao,” anasimulia kwa huzuni Mashele.
“Maji yalikuwa mengi usawa wa nusu ya ukuta na yalikuwa na kasi, wakati wakijaribu kumpandisha (Theresia) kwenye ngazi, iliteleza na kuwasomba wote watatu yaani Theresia, Ally na Mbwela (aliyenusurika).
Mashele alisema baada ya kusombwa wote, wananchi waliokuwapo waliendelea kupiga kelele lakini walishindwa kutoa msaada wowote kutokana na maji hayo kuwa na kasi kubwa.
Alisema kwa mbali baadhi ya wananchi waliokuwapo walimuona Mbwela akijaribu kujiokoa kwa kushika miti iliyokuwa pembezoni mwa Mto Bumbulu yalikokuwa yakielekea maji hayo.
“Baada ya saa moja waliona Mbwela akiwa amenasa kwenye mti jirani na eneo la nyumba hiyo akiwa hai na juhudi zilifanyika ili kumuoka, ilipofika saa nane mchana maji yalipungua na waliweza kumtoa akiwa bado hai.”
Alisema baada ya wawili hao kutoonekana, wananchi walianza juhudi za kuwatafuta.
Mwili wa Theresia ulipatikana juzi saa mbili usiku ukiwa unaelea juu ya maji katika mto huo na mwili wa Ally ulipatikana jana saa saba mchana ukiwa umenasa kwenye mti ndani ya bonde la mto huo.
Kwa upande wa familia ya marehemu Ally, mdogo wake Innocent Ambrose alisema wakati mvua inanyesha saa nne asubuhi walisikia kelele kutoka nyumba ya jirani ndipo kaka zake wawili Mbwela na Ally wakatoka kwenda kuona kinachoendelea.
Alisema walipofika walikuta nyumba ya jirani yao imejaa maji hivyo kaka zake hao waliingia katika nyumba hiyo ili kuwaokoa.
Ambrose alisema kaka yake (marehemu Ally) alikuwa ni askari wa Suma JKT na alikuwa kwenye maandalizi ya kufunga ndoa.
Diwani wa Kata ya Kiluvya, Aidan Kitare alisema amesikitishwa na tukio hilo, ambalo limesababisha wananchi wake wawili, Ally na Theresia kufariki dunia.
“Nitumie nafasi hii kuwaomba wananchi wa Kiluvya na Watanzania kuwa makini wapitapo karibu na kingo za mito na madaraja, lakini zaidi ya yote tuwachunge watoto,” alisema.
Pia aliwataka wananchi kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa ambazo zinatolewa na mamlaka ya hali ya hewa kwa lengo la kuchukua tahadhali.     

No comments:

Post a Comment