Sunday, October 1

Chadema ‘yatema’ saba Kusini

Mwenyekiti wa kanda hiyo ambaye pia ni Mbunge
Mwenyekiti wa kanda hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe 
Chama cha Democrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kusini kimewavua uanachama wanachama saba huku wengine watatu wakitakiwa kutojihusisha na shughuli za chama kwa muda wa miezi 30 kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utovu wa nidhamu.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Kanda, mwenyekiti wa kanda hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe amesema baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Ruvuma ikiwemo Songea Mjini walivuliwa uongozi kwa ngazi ya wilaya hadi mkoa kutokana na  utovu wa nidhamu.
Mwenyekiti huyo amewataja waliovuliwa uanachama huo kuwa Joseph Kwime, Emmanuel Karisinje, Roda Komba, Seifu Ahmed Seif, Suwedi Millanzi, Mustafa Songambele na Ajaba Nditi.
“Sisi kama kanda tulipelekea taarifa kwao tukiamini kwamba watakuja kukata rufaa kwetu kwamba hawakuridhika na hatua ambazo zimechukuliwa lakini hawakufanya hivyo basi kamati tendaji ikaridhia kuvuliwa uanachama kwa wanachama hao,”amesema Mwambe
Amesema ambao wametakiwa kutojihusisha na shughuli za chama kwa muda wa miezi 30 ni pamoja na Zuberi Tendwa, Sikitu Salum na  Halifa Jafa huku Katibu wa Chadema Wilaya ya Nachingwea, Juma Chitende akivuliwa nyazifa ya uongozi na kubakia kama mwanachama wa kawaida.
“Ni bora tuanze upya kuliko kuwaacha watu wachache ambao watatuharabia mipango yetu ya chama wakati tukiweka mikakati kuelekea mwaka 2020 ndiyo maana wanachama kama hao tumeamua kuwavua nyazifa zao ili tuweze kusonga mbele.”

No comments:

Post a Comment