Wanasiasa wawili nchini Kenya wamekamatwa na kuhojiwa na maafisa wa polisi kwa tuhuma za kutoa matamshi ya kueneza chuki na uhasama wa kikabila nchini humo.
Msemaji wa wizara ya ndani nchini humo, amesema kwamba, mbunge wa Gatundu Kusini, anakotoka Rais Uhuru Kenyatta, Bw Moses Kuria, na ambaye ni mwanachama wa chama tawala cha Jubilee pamoja na mwenzake wa muungano wa upinzani National Super Alliance Nasa, Johnston Muthama, kwa sasa wanazuiliwa na maafisa wa polisi.
Baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali ushindi wa Bw Kenyatta, Bw Kuria aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba kutafanywa msako wa kuwawinda waliyempigia kura "shetani huyo".
"Kiambu imezungumza. Imesema Wembe ni ule ule. Wangige na Kiambu [ ngome za Bw Kenyatta] watu wamekasirika sana.
"Kura zao milioni moja zilibatilishwa na watu wanne (majaji wa Mahakama ya Juu). Lakini wako tayari sana kurudia na kupiga kura. Na hata zaidi. Msako utafanywa usiku kuwatafuta 200,000 ambao hawakupiga kura na wengine hao 70,000 waliompigia kura "shetani huyo mwingine."
Katibu mkuu wa chama cha Jubilee chake Bw Kuria, Bw Raphael Tuju, alishutumu ujumbe huo wa mbunge huyo wa Gatundu Kusini na kusema haukubaliki.
Bw Muthama, ambaye alikuwa seneta wa jimbo la Machakos katika bunge lililopita lakini hakutetea wadhifa huo uchaguzini, naye anadaiwa kuandamwa kutokana na ujumbe alioutoa katika mkutano wa kisiasa mwishoni mwa wiki.
No comments:
Post a Comment