Sunday, September 17

‘Wahitimu wanaoingia kwenye soko la ajira wana ujuzi hafifu’

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Mary Kawar kitabu cha Miongozo ya Mafunzo Katika Maeneo ya Kazi wakati wa uzinduzi uliofanyika mjini Dodoma jana. Katikati ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana , Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu 
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa waajiri nchini kuwa wahitimu wengi wamekuwa wakiingia katika soko la ajira wakiwa hawana ujuzi unaohitajika na hulazimika kuajiri wafanyakazi kutoka nje ya nchi.
Akizungumza katika uzinduzi wa mafunzo ya uanangezi na mafunzo kazini, Majaliwa alisema kuwa katika kutatua changamoto hiyo waliamua kuandaa programu maalumu ya kukuza ujuzi.
Majaliwa alisema Serikali ilijadiliana na wafanyakazi, waajiri na kukubaliana kuwa kuna haja ya kuchochea na kuimarisha mfumo wa utoaji wa mafunzo yanayofanyika maeneo ya kazi.
“Kwa pamoja tulianzimia kuandaliwa kwa miongozo ya kitaifa ya kusimamia mafunzo ya vitendo kwa wahitimu na mafunzo ya uanagenzi lengo kuhakikisha mafunzo yanayotolewa maeneo ya kazi yana ubora unaohitajika,”alisema.
Alisema Serikali kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 iliandaa kuanza kutekeleza programu ya miaka mitano ya Taifa ya kukuza ujuzi ambayo itatoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa takribani milioni 4 ili kuziba pengo la ujuzi lililopo nchini kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi wa mwaka 2014.
Alisema katika mwaka wa fedha 2016/17 kupitia programu hii wamewezesha kutolewa mafunzo kwa vijana 11,340 katika fani mbalimbali kupitia vyuo vya mafunzo vya umma na binafsi.
Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye ulemavu, Jenista Mhagama alisema programu hiyo iliyoanza 2015/16 imekuwa na mwitikio mdogo wa wadau kwa sababu ya kukosa miongozo hiyo.
“Miongozo hii imeweka bayana utaratibu wa kugharamia mafunzo ukiwa ni pamoja kuwashirikisha Serikali na waajiri, pia imeweka bayana vigezo vya kuwapata washiriki wa mafunzo na muda maalum wa mafunzo,”alisema.
Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO), Gerald Runyoro alisema zaidi ya vijana milioni moja wanamaliza elimu katika vyuo lakini wanaopata ajira katika sekta rasmi hawazidi 200,000.
Alisema katika programu hiyo inalenga katika kuwaunganisha kwa pamoja wahitimu hao na wajasiriamali wadogo na wa kati kuona kama wanaweza kufanya kazi pamoja.
“Katika programu hii tuligundua kuwa wahitimu wanafikiri wajasiriamali hao hawahitaji elimu kama yao na wajasiriamali wanafikiri hawawezi kufanya kazi nao na wanahitaji mishahara mikubwa,”alisema.
Alisema walipata wahitimu 400,000 waliokuwa tayari kushiriki katika mafunzo kwa vitendo lakini nafasi zilizopatikana zilikuwa 224.
Alisema katika programu hiyo ya miezi mitatu na nusu walifanikiwa kupata ajira kwenye sekta rasmi na wengine hawakupata huku wengine wakiishia njiani baada ya kupata ajira.
Alisema wajasiriamali walionyesha kufaidika na programu hiyo na wahitimu kupata ujuzi unaowawezesha kufanya kazi zao kiufanisi.
Mkurugenzi wa Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) kwa nchi za Tanzania, Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda, Dk Mary Kawar alisema shirika hilo liko tayari kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuhakikisha programu hiyo inafanikiwa.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Yahaya Msigwa alishauri Serikali kuihamishia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) ili kuongeza ufanisi katika mafunzo kazini.
Alisema kuwa Veta kuwekwa chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kunavifanya vyuo vya Veta kujielekeza zaidi katika taaluma kuliko mafunzo kwa vitendo.
“Wizara ya Elimu imeelemewa tuitoe na kuepeleka wizara ya kazi kama ilivyokuwa huko nyuma. Stadi za kazi ni zaidi ya taaluma,” alisema.

No comments:

Post a Comment