MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ameteua Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Queen Mlozi kuongoza Kamati aliyoichagua kwa ajili ya kufuatilia viwanda mbalimbali ili kuangalia hali halisi na kama vimeshindwa kufanyakazi viweze kupewa Wawekezaji wengine. Mwanri aliteua Kamati hiyo jana mjini Tabora wakati wa Mkutano na wadau mbalimbali na Mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi cha Tabora.
Wengine waliochaguliwa ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Tabora Dkt. Philipo Ntiba, Afisa Biashara Mkoa Lucas Kusare ambaye ni Katibu wa Kamati, Mwanasheria wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Richard Lugomela na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini, Tiganya Vincent.
Alisema kuwa Kamati hiyo itaanza na Kiwanda cha Nyuzi Tabora ambapo itaangalia mpango kazi wake , itakagua mashine zote kama zinafanyakazi na uwezo wa kifedha wa mwekezaji huyo kama anao mtaji wa kutosha wa kuendesha kiwanda.
Mambo mengine yatakayofuatiliwa na Kamati hiyo ni pamoja na kuangalia matatizo ambayo Mwekezaji huyo aliyaeleza kuwa ukosefu wa soko la nyuzi zake kutokana na viwanda ambavyo ndio vilikuwa vikinunua kwake kuanza kuagiza toka nje bidhaa hizo.
Mkuu huyo Mkoa aliongeza kuwa mambo mengine ambayo Kamati itayafanya ni kuangalia fursa za masoko ya bidhaa za Kiwanda hicho kama vile Bohari Kuu za Dawa (MSD), Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU) na wafanyabiashara wengine wanaweza kununua bidhaa zake.
Alisema kuwa Kamati hiyo itatakiwa kila baada ya siku tatu impelekee taarifa ya maendeleo ya kazi yao.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ametoa mwezi mmoja kwa Mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi Tabora kuhakikisha mashine zake zinafanyakazi.
Alisema kuwa baada ya kipindi kuisha atakwenda kukagua na akikuta hakuna kitu atalazimika kumuomba Waziri wa Viwanda aje kuchukua hatua ikiwemo kumpa mwekezaji mwingine.
Mkuu huyo Mkoa alisema kuwa hata kama mali ghafi kwa sasa hivi hakuna anataka ni kujiridhisha kuwa mashine zote ni zima wakati akiwa anasubiri msimu wa pamba ujao ili apate mali ghafi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora yuko katika zoezi la kuhakiki viwanda vyote ili kujiridhisha kama vinafanyakazi na vile ambavyo wamiliki wake wameshindwa waweze kuvirudisha Serikalini
No comments:
Post a Comment