Saturday, September 30

Magufuli anavyoua ndege wawili kwa jiwe moja




Kikatiba, Rais wa Tanzania amepewa mamlaka ya kuwa Mkuu wa Nchi, Kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Majukumu hayo huyatekeleza kulingana na mahitaji ya wakati husika.
Kwa upande mwingine, Rais anayetokana na CCM, hubeba pia madaraka ya mwenyekiti wa chama kama msimamizi mkuu wa ilani ya chama.
Kutokana na kofia hizo mbili, Rais wa sasa na wengine waliomtangulia wamekuwa wakilalamikiwa kwa kuchanganya matukio ya chama na Serikali.
Wamekuwa wakidaiwa kutumia mamlaka yao ya kiserikali kujenga chama, fursa ambayo vyama vingine vya siasa havina, hasa mbali na kipindi hiki ambacho vinazuiwa kufanya shughuli za kisiasa.
Licha ya Rais sasa, John Magufuli kusisitiza kuwa yeye ni Rais wa Watanzania wote bila kubagua vyama, dini au makabila yao, katika baadhi ya matukio ya Kiserikali ameonekana kufanya siasa zinazoviathiri vyama vingine ambavyo havina fursa ya kujibu mapigo.
Wiki iliyopita ameonekana akiwatega kwa mafumbo wabunge sita wa vyama vya upinzani kuhama vyama vyao, huku akipokea madiwani waliohama kutoka Chadema kwenda CCM.
Katika baadhi ya ziara zake za kiserikali, Rais Magufuli amekuwa akisikika akisema, “Huyu ingawa ni upinzani lakini damu yake ni CCM katikati ya matukio la uzinduzi wa miradi ya maendeleo, shughuli za kiserikali au wakati wa kushukuru wananchi kwa kumchagua.
Wachambuzi wa duru za kisiasa wanasema athari za kauli hizo za mara kwa mara ni kuvidhoofisha vyama vya upinzani ili wananchi wasiwakubali katika uchaguzi ujao.
Hata hivyo, utaratibu huo unatetewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole kuwa Rais kwa asili yake kikatiba ni mwanasiasa namba moja kama ilivyo Mtanzania namba moja Tanzania.
“Amechaguliwa na akapewa nafasi tatu ambazo ni mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amri Jeshi Mkuu. Nafasi ya kiongozi wa Serikali ni nafasi ya kisiasa, ambayo amechaguliwa na wananchi, akiwa msimamizi wa sheria, sera, mikakati na mipango ya Serikali.
 “Kwa hiyo Rais anapopita barabarani, anakuwa na kofia tatu. Wako watakaomtazama kama mkuu wa nchi, wengine wanamwona ni kiongozi wa Serikali na wengine kumtazama kwa kofia zote tatu. wananchi wakimwona wakati wowote watajitokeza kupelekea kero, kuomba msaada au kumsikiliza,” anasema.
Anasema wananchi pia wanafahamu kazi anazofanya Rais Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho ni maelekezo ya chama, hivyo wanaojitokeza kujiunga na CCM hupendezwa na kazi anazofanya.
“Wapo watu wameona kazi za Rais, kwamba anachokifanya, anakifanya kwelikweli, amezungumza mipango, mikakati, kama ni rushwa, ameishughulikia, wanaamua kujitokeza kwenye mikutano na kusema huku tuliko ni mizengwe, tunaona tuje tuunge mkono kazi unayoifanya wewe (Rais Magufuli), sasa unataka awafukuze?” anasema.
Polepole aliyekuwa anatolea ufafanuzi tukio la aliyekuwa Diwani wa Kimandolu (Chadema), Mchungaji Rayson Ngowi kujitokeza wakati Rais Magufuli akitunuku Kamisheni kwa maofisa 422 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jijini Arusha, anasema matukio hayo hayaandaliwi na chama bali hujitokeza siku ya tukio.
Katika mkutano huo, Rais Magufuli aliuliza kama kuna mwanachama yeyote anayetaka kujiunga na chama hicho au kukihama, ajitokeze mbele.
“Hakuna utaratibu uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya kupokea wanachama wapya siku hiyo, nilikuwapo. Taratibu za chama zinataka kuandikishwa uanachama katika ngazi ya tawi lako, lakini Rais ana mkutano huko na watu wakamwambia sisi tunataka tuondoke huku tuliko, unataka awakatae pale mkutanoni?” anasema.
Anafafanua kuwa diwani huyo wa Kimandolu aliamua kukata shauri mwenyewe pale mkutanoni baada ya kujiuzulu. Anasema Rais hakuomba ila kuna itifaki iliyomsaidia na hakuna aliyekuwa anafahamu.
Hapana shaka kwamba mkuu wa nchi kujihusisha na kauli au matukio ya kukipigia debe chama chake na kuingiza wanachama wapya kwenye matukio ya kiserikali yanalenga kukiimarisha na kukiepusha na kuporomoka.
Hii ni kutokana na takwimu kuonyesha kuwa ushawishi wake unazidi kupungua. Mwaka 2005 Rais mstaafu, Jakaya Kikwete alipata ushindi wa asilimia 81 lakini mwaka 2010 akafikia asilimia 61. Mwaka 2015 Rais Magufuli aliibuka na asilimia 58.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda anasema kuwa chama kinaweza kuporomoka zaidi endapo hakitafanya jitihada za kuongeza wanachama wapya na kuongeza nguvu ya ushawishi wa kisiasa kupita kundi la vijana.
Mapambano na wapinzani
Pamoja na kauli kwamba baadhi ya wapinzani wana damu ya CCM katika kipindi ambacho wapinzani hawaruhusiwi kufanya mikutano ya hadhara, akiwa katika majimbo yanayoshikiliwa na upinzani kila alipopokea kero kutoka kwa wananchi, Rais Magufuli amekuwa anachomekea kauli za kuwabeza au kuwataka wananchi wasifanye tena makosa.
Julai 23, Rais Magufuli alimpongeza Magdalena Sakaya (Kaliua-CUF) kwa ushirikiano wake katika shughuli za maendeleo huku akisema ingawa kimwili mbunge huyo ni CUF, lakini damu yake na roho yake ni vya CCM.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kaliua, Tabora wakati wa ufunguzi wa Barabara ya Kaliua – Kazilambwa, kwenye Uwanja wa Kasungu.
Magufuli alisema Sakaya amekuwa akifanya kazi nzuri za maendeleo katika kutekeleza ilani ya CCM, bila kuwabagua kwa itikadi ya vyama vyao na akawataka wanaCCM kushirikiana naye.
“Mheshimiwa Sakaya ukimwangalia mwili wake ni mwana-CUF, lakini damu yake na roho yake ni mwana CCM. Inawezekana siku moja akahamia CCM.
“Ni bora kuwa na mwanaCUF, au mwana Chadema, au mwana-ACT anayefanya kazi za CCM kuliko kuwa na mwana CCM anayefanya kazi za chama kingine. Si mmenielewa? Mimi najua, maana hata wakati wa kampeni niliyaona.”
Mbali na Sakaya, Rais Magufuli Julai 22, mwaka huu alimshtaki Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago kwa wapigakura wake kwamba, wananchi wa eneo hilo wanateseka kutokana na makosa ambayo waliyafanya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Akiwa katika Jimbo hilo, Rais Magufuli aliwapiga vijembe wapigakura akisema mbunge wa hapo (Bilago), aliwaahidi wananchi kwamba angemaliza suala la maji na kuwahoji, “Leo amelimaliza?” akajibiwa badoo. Kisha akasema ndiyo mjifunze sasa.
Kutoka na kauli hiyo ya Rais, Bilago anasema ilimlazimu kufanya ziara katika kata zote 13 za jimbo lake ili kujitetea mbele ya wapigakura wake. Alisema Rais Magufuli alikosea kuwaambia wananchi wasimchague tena katika uchaguzi ujao kwa kigezo cha kero ya maji kwani kazi ya mbunge siyo kupeleka maji, umeme wala kujenga barabara.
“Wapo walionipigia simu wakihoji juu ya kauli hiyo ya Rais, nikawaelewesha, wengine walielewa palepale na wengine ilibidi niwazungukie kwenye kata kuwaelewesha. Wananchi wanatakiwa kujua mbunge hawezi kuleta maji, mbona mbunge wa CCM hakuwaletea maji? Hili ni tatizo la utawala uliopo,” alisema.
Mbali na Buyungu, akiwa Tanga Mjini, Rais Magufuli alimkaribisha CCM mbunge wa jimbo hilo anayetokana na CUF, akitumia ufafanuzi wa CCM kama nyumba kubwa yenye lango la kuingia.
“Njia ya kuingia kwenye linyumba la CCM ambalo ni likubwa, nyumba ya wengi, kwa hiyo nyumba ipo na unakaribishwa kuingia kwenye nyumba hii ya CCM,” alisema.
Lakini mbunge huyo, Mussa Mbarouk anasema yeye bado ni CUF na hafikirii kuingia nyumba ya CCM kutokana na imani iliyojengwa na wananchi wa jimbo lake kupitia CUF.
“Najua Rais ananihitaji sana CCM na baada ya kauli yake yaliibuka makundi mawili; kundi lililoamini ni utani na lingine ndani ya chama wakihofia nitawasaliti. Maneno ya kunituhumu kwa wapinzani ndani ya chama yalianza kutolewa lakini nikawatoa hofu kwamba kimwili na kimoyo niko CUF,” anasema Mbarouk.
Machi 3, Rais Magufuli alimweka katika wakati mgumu mbunge wa Kilwa Kaskazini (CUF), Vedasto Ngombale mbele ya wapigakura wake baada ya kumtaka achangie Sh15 milioni kutoka mfuko wa jimbo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya, lakini mbunge huyo akasema hawezi kutoa ahadi ambayo hataitekeleza.
Tukio hilo lilitokea eneo la Somanga Wilaya ya Kilwa wakati Rais aliposimama kuwasalimia wananchi ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mikoa ya Kusini. Katika tukio hilo, Rais Magufuli alikuwa akimuuliza maswali ya mtego, huku akisisitiza umuhimu wake kama mbunge kuchangia ujenzi huo. Rais aliahidi kuchangia Sh20 milioni.
Mbunge huyo anasema baada ya kauli hiyo ya Rais ilimlazimu kufanya mikutano katika kata za Kinjumbi na Namayuni kuwaweka sawa wapigakura wake.
“Wapo ambao hawakuelewa pale na ndiyo maana niliamua kufanya mikutano, maana ilionekana Rais ndiye mwenye msaada na mimi sina umuhimu. Niliwaeleza kuwa fedha za mfuko si za mbunge na zina utaratibu wa kutolewa. Nina kata 13, vijiji 54, isingewezekana kutoa Sh15 milioni kwenye mradi mmoja kati ya Sh36 milioni zilizokuwa zimebakia,” anasema.

No comments:

Post a Comment