Saturday, September 30

Lissu atakuwa mkubwa zaidi akitoka hospitali


Zipo tafsiri mbili katika tukio la mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kunusurika katika shambulio la risasi. Ya kwanza ni ya kibinadamu, kwa maana ya fikra za kawaida, ya pili ipo kiroho, kwa kuzielekea kudura za Mwenyezi Mungu.
Tafsiri ya kibinadamu inaweza kuwa na matawi mawili, la kwanza ni kuwa aliyemlenga na kumiminia Lissu risasi hana shabaha, kwa hiyo hakumpatia eneo nyeti. Tawi la pili ni kwamba kwenye gari kulikuwa na giza, hivyo mlenga shabaha alipiga tu kwa kubahatisha.
Tafsiri ya kiroho ina maeneo mawili, kwamba siku ya Lissu ilikuwa haijafika au Mungu alikuwa hajaafiki kumtwaa. Ni maneno yenye mantiki sawa, lakini nyongeza ya hapo kiroho ni kuwa Mungu bado anao mpango wa kidunia na Lissu, hivyo amekataa kumtwaa ili agano litimie.
Lissu alishambuliwa na watu ambao mpaka leo hawajafahamika ambao bila shaka lengo lao lilikuwa kumuua Lissu, walipomaliza shambulio lao walikimbia.
Tukio lilitokea Septemba 7, mwaka huu, mchana alipowasili nyumbani kwake kutoka bungeni.
Ukuu ndani ya Lissu
Nashika ile tafsiri ya kiimani kuwa Mungu hakutaka Lissu afe. Siku yake bado haijafika. Mungu ana mpango mkubwa naye ambao hawezi kuruhusiwa kuiacha dunia kabla hajautimiza. Hivyo basi, upo ukuu ndani ya Lissu ambao utadhihirika baada ya kutoka hospitali.
Wakati ukitembea na imani kuhusu mpango wa Mungu kwa Lissu, tafsri pia ya tukio lake, kushambuliwa kwake na jinsi alivyopona kuoanisha na matukio ambayo yamewahi kutokea. Kuna watu wengi wamefanya makubwa duniani baada ya kupona katika shambulio la risasi.
Katika kutazama watu wakubwa waliotikisa duniani baada ya shambulio la risasi, utaona kuwa wapo ambao walipigwa risasi za kichwa lakini walipona. Ni hapo utauona uamuzi wa Mungu, anapoamua kukataa kutoa kibali cha kutenganisha nafsi na mwili wa mja wake.
Kwa yule ambaye anaamini kuwa Lissu amenusurika kifo kwa sababu ya maeneo ambayo risasi zilipigwa, mimi naweza kumuuliza; ilishindikana nini risasi kupenya kwenye mwili wa Lissu na kufumua moyo? Ni Mungu tu!
Hapo utaona kuwa ipo kinga iliyokuwapo. Wale waliomshambulia hawakuwa na kibali cha kumuua. Gari la Lissu halikuwa na uwezo wa kuzuia risasi lakini amenusurika.
Mungu akiamua huzuia kifo kwa yeyote hata kama atakuwa anaonekana yupo jirani na kifo kiasi gani. Ni utaratibu uleule ambao Mungu aliufanya kumuweka hai Yona ndani ya tumbo la samaki baada ya kumezwa, ndiyo ambao huutumia kuwalinda waja wake ambao bado wana kazi hawajaimaliza.
Yona ambaye kwenye Kuran anatamkwa Yunus, alikuwa anakimbia jukumu la kueneza neno la Mungu. Akiwa anakimbia alikutana na changamoto ya usafiri majini. Baada ya chombo kupata dhoruba, ilibidi Yona atoswe majini. Akamezwa na samaki lakini alitemwa nchi kavu akiwa mzima baada ya siku tatu.
Mifano imekuwa mingi
Oktoba 9, 2015, msichana Malala Yousafzai, raia wa Pakistan akiwa na umri wa miaka 15, alipigwa risasi ya kichwa na mtu mwenye bunduki ambaye inaamika alikuwa mwanamgambo wa Taliban.
Malala akiwa kwenye gari na wanafunzi wenzake, mtu mwenye bunduki aliingia na kutaka msichana huyo ajitambulishe. Baada ya Malala kujitambulisha, alimpiga risasi ya kichwa na kuondoka akidhani amemuua. Baadaye Malala alipelekwa hospitali na kupona.
Sababu ya Malala kupigwa risasi ilikuwa harakati zake za kutaka mtoto wa kike apate haki sawa ya kielimu. Alipaza sauti na alitoa elimu ambayo iliwafikia wengi. Harakati zake ziliwakera Taliban na kutaka kummaliza.
Malala mwenye umri wa miaka 20 hivi sasa, amekuwa mwanaharakati mashuhuri na shujaa wa mtoto wa kike ulimwenguni. Kupitia Malala unaweza kupata ile tafsiri kwamba Mungu alikuwa bado na kazi naye.
Mwaka 2013, Malala aliandika kitabu kinachoitwa I am Malala (Mimi ni Malala) ambacho kimekuwa kielelezo cha ukombozi wa mtoto wa kike ulimwenguni. Kwa kifupi ni Malala amekuwa mkubwa baada ya kunusurika kifo.
Mei 1981, aliyekuwa kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa John Paul II alishambuliwa kwa risasi na kudhaniwa angekufa. Katika shambulio hilo, ilikadiriwa kuwa Papa alipoteza kiasi cha robo tatu ya damu mwilini.
Papa alitibiwa na kupona. Baada ya hapo aliliongoza Kanisa Katoliki kwa miaka 24 kabla ya kufariki dunia mwaka 2005. Mpaka sasa, Papa John Paul II ameweka rekodi ya kuwa Papa wa tatu kuongoza Kanisa Katoliki muda mrefu zaidi. Akiwazidi wote katika Karne ya 20 na 21.
Papa aliyeliongoza Kanisa Katoliki kwa muda mrefu zaidi ni Mtakatifu Petro, aliyehudumia miaka 35 katika Karne ya Kwanza na anayemfuatia ni Blessed Pius IX, aliyeongoza kwa miaka 32 katika Karne ya 19.
Hivyo basi, kumekuwa na ushuhuda mzuri wa watu ambao wamepata mafanikio makubwa baada ya kupona shambulio la risasi.
Miujiza baada ya risasi
Mwanamuziki wa Hip Hop nchini Marekani aliye mashuhuri ulimwenguni kote, Curtis Jackson ‘50 Cent’, alishambuliwa kwa risasi mwaka 2000 na tisa ziliingia mwilini. Aliumizwa usoni hadi kuvunjwa gego. Alijeruhiwa miguu, mikono na kiuno.
Wakati 50 Cent anajeruhiwa hakuwa na umaarufu wowote. Alikuwa mwanamuziki asiyefahamika, huku akihangaika kutambulika kwenye soko la muziki. Mwaka 2001 ulimkuta akiendelea kuuguza majeraha yake hayo.
Mwaka 2002 akiwa ameshapona, kipaji chake kilivumbuliwa na mwanamuziki mkubwa wa Hip Hop, Marshall Bruce Mathers III ‘Eminem’ ambaye aliingia naye mkataba wenye thamani ya dola 1 milioni ambazo kwa wakati huo zilikuwa sawa na Sh1 bilioni.
Mwaka 2003, 50 Cent alitoa albamu yake ya kwanza inayoitwa Get Rich Or Die Tryn’ ambayo iliuza zaidi ya nakala 14 milioni kisha mwaka 2015 alitoa albamu ya pili inayoitwa The Massacre iliyouza nakala 15 milioni. Albamu hizo mbili zilimpa daraja kubwa mwanamuziki huyo na kufanya mauzo ya kihistoria.
Miujiza hiyo ya mafanikio baada ya shambulio la risasi ipo pia kwa mwanamapinduzi wa Hip Hop Marekani, Tupac Shakur aliyepigwa risasi tano mwaka 1994 lakini alipona. Risasi mbili zilimjeruhi kichwani, nyingine kifuani, mkononi, pajani na mguuni.
Wakati Tupac anafanyiwa shambulio hilo, alikuwa ameshauza nakala takriban milioni tatu kupitia albamu zake mbili alizorekodi kama mwanamuziki binafsi, na nyingine moja aliyofanya na kundi lake la zamani la Thug Life.
Tupac baada ya kunusurika na shambulio hilo, alifanya maajabu kwa kurekodi nyimbo ambazo zimewezesha albamu 11 hadi sasa. Mpaka alipouawa kwa shambulio lingine la risasi Septemba 1996, alikuwa ameshatoa albamu nne tu kama msanii binafsi.
Ni Tupac aliyeweka rekodi ya kuwa mwanamuziki wa Hip Hop aliyeuza nakala 75 milioni katika albamu zake. Rekodi ambayo ilivunjwa na Eminem aliyefikisha nakala 80 milioni. Hesabu ni kuwa nakala zaidi ya 70 milioni za Tupac zilitokana na kazi alizofanya baada ya kunusurika kifo kwa shambulio la risasi.
Kwa wadau wa muziki wa Reggae, wataelewa rekodi ya mauzo ambayo nguli Bob Marley aliiweka kupitia albamu yake Exodus akiwa na bendi yake ya The Wailers. Albamu hiyo ilitoka mwaka 1977 baada ya Bob Marley kujeruhiwa kwa risasi mwaka 1976. Exodus iliuza nakala zaidi ya 70 milioni.
Kimsingi baada ya Marley kunusurika shambulio la risasi mwaka 1976, alitoa albamu tano zilizokuwa na mafanikio makubwa, ikiwemo Legend ambayo ndiyo rekodi mbalimbali za mauzo zinaitambulisha kuwa namba moja katika albamu zote za Reggae kuwahi kutokea.
Ongeza na mfano wa Rais mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo, mwaka 1996 akiwa na rafiki yake, Shehu Yar’Adua, walihukumiwa kifo na Mahakama ya Kijeshi, Nigeria.
Baadaye adhabu hiyo ikabadilishwa kuwa kifungo cha miaka 30 jela. Mwaka 1997 Yar’Adua alifia gerezani. Mwaka 1998 Obasanjo aliachiwa huru. Mwaka 1999 Obasanjo akachaguliwa kuwa Rais wa Nigeria.
Mifano hiyo ndiyo ambayo inathibitisha kuwa Mungu anapomnusuru mja wake na jaribio zito la mauti, baadaye mja husika hupanda daraja kubwa. Maana humnusuru ili atimize agano. Ni uthibitisho huo unaonifanya nimuone Lissu mtu mkubwa zaidi ya sasa baada ya kutoka hospitali.

No comments:

Post a Comment