Tuesday, September 12

Dk Mashinji aeleza jinsi risasi zilivyomvunja Lissu



Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji 


Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu ameumizwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake na kwamba alipigwa risasi nyingi tofauti na risasi tano zilizoelezwa.
Dk Mashinji amesema Lissu amevunjwa miguu yake, nyonga na mkono wa kushoto, jambo ambalo linawapa madaktari kazi kubwa na kuimarisha afya yake.
Kiongozi huyo amesema jana asubuhi Lissu alianza kusumbuliwa na kifua, jambo lililowalazimu madaktari kumwekea mashine za kumsaidia kupumua, hata hivyo anasema walizitoa baadaye na leo Jumanne ameamka salama.
"Bado najisikia uzito kuelezea hali ya Tundu Lissu. Kwa namna alivyoumia inawezekana matibabu yakachukua muda mrefu, hivyo tuendelee kumwombea na kuchangia matibabu hayo," amesema Dk Mashinji.
Amesema Lissu ameongezewa damu nyingi akiwa Dodoma na bado anaendelea kuongezewa huko Nairobi. Amesema madaktari wanajitahidi kuokoa maisha yake na kwamba ana imani kwamba watafanikiwa.
"Sasa hivi wamemtibu sehemu za ndani ambazo zingehatarisha uhai wake, hilo wamemaliza sasa wameanza sehemu za nje na mpaka sasa amefanyiwa operesheni tatu. Madaktari wamesitisha kumfanyia upasuaji kwanza ili apate muda wa kupumzika."
"Tutatumia resource(rasilimali) zote tulizonazo kama chama kuhakikisha tunaokoa uhai wake," amesema Dk Mashinji mbele ya vyombo vya habari na wanachama waliohudhuria mkutano huo.

No comments:

Post a Comment