Rais Jacob Zuma amesema amepokea na kuridhia uamuzi wa kujiuzulu kwa Naibu Waziri wa Elimu ya Juu na Mafunzo, Mduduzi Manana.
“Rais amemshukuru Manana kwa mchango wake katika kipindi alichokaa ofisini,” ilisema taarifa fupi ya Ikulu mwishoni mwa wiki.
Manana amejiuzulu siku chache baada ya kukiri kuwashambulia wanawake wawili katika klabu ya usiku ya Cubana iliyoko Fourways, Johannesburg. Alhamisi iliyopita Manana alifikishwa katika Mahakama ya Randburg ambako anakabiliwa na mashtaka mawili ya kusudio la kudhuru mwili na aliachiwa kwa dhamana ya Randi 5,000.
Aidha, chama tawala cha ANC kimempongeza naibu waziri huyo kwa uamuzi wa kujiuzulu na pia kimempongeza kwa kipindi chote alichoitumikia Serikali. Manana anakabiliwa na hatua za kinidhamu kwenye chama hicho.
No comments:
Post a Comment