Pengine imeanza kuzoeleka na haionekana kama tena ni jambo la kushtua kusikia kiongozi wa juu wa Chadema amekamatwa au kulala mahabusu.
Chadema kimetaja vigogo wake wanne ambao wamekuwa wakipishana mara kadhaa katika korido za vituo vya polisi nchini kwa tuhuma mbalimbali.
Anayeongoza katika hilo ni mwanasheria mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu ambaye ameshaingia katika mikono ya polisi mara nane.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki anafuatiwa na Mbunge wa Kawe Halima Mdee ambaye amefikisha mara saba.
Vigogo wengine wawili, mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa wamefungana kwani kila mmoja ameripoti polisi mara tano katika vipindi tofauti.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema matukio hayo yamejitokeza katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu na sehemu kubwa ya makosa yaliyowafikisha katika maeneo hayo ni kutoa kauli za uchochezi, kuendesha mikusanyiko isiyoruhusiwa kisheria na kuhusishwa katika mtandao wa dawa za kulevya.
Lissu ambaye juzi alikamatwa na maofisa wa polisi Kituo Kikuu Dar es Salaam pia ndiye anayeongoza kulala mahabusu kwa mara nyingi mara nyingi amekuwa akidaiwa kutoa kauli za uchochezi, mikusanyiko isiyokuwa halali. Amekamatwa mara mbili akiwa mkoani Singida na mara sita akiwa jijijni Dar es Salaam.
Juzi, alikamatwa kwa kosa la kutoa kauli za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli ikiwa ni siku chache baada ya kuibua sakata la ndege ya Bombardier kuzuiwa nchini Canada.
Mwanasiasa huyo aliwahi kusema mahabusu siyo mahali pa zuri na hapendi hali hiyo ijitokeze lakini yuko tayari kwenda endapo kauli alizodai ni za kuikosoa Serikali zitakuwa kigezo.
Mdee amewahi kufunguliwa mashtaka ya jinai na kulala mahabusu kwa kesi mbalimbali ikiwamo sakata la uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Operesheni Ukuta akiwa na viongozi wengine na kauli za uchochezi, hatua iliyomfikisha mara saba katika maeneo hayo.
Mbowe, amewahi kuhojiwa kupitia sakata la dawa za kulevya, Operesheni ya Ukuta na kutoa kauli za uchochezi ambayo kwa ujumla yalimfikisha mara tano katika vituo vya polisi.
Julai 20, Lowassa aliripoti makao makuu ya Jeshi la Polisi ikiwa ni mara ya nne akituhumiwa kutoa kauli za kichochezi wakati wa futari iliyoandaliwa Juni 23, na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara.
Katika futari hiyo, Lowassa anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi kuhusu masheikh wa Taasisi ya Uamsho wanaoshikiliwa gerezani akidai utaratibu wa kisheria ufanyike ili waachiwe huru.
Pia, Agosti 30 mwaka jana, Lowassa akiwa na viongozi wengine wa Chadema walikamatwa wakifanya mkutano katika Hoteli ya Girrafe, Dar es Salaam. Wengine walikuwa Mbowe, Dk Mashinji, John Mnyika na Said Issah.
Julai mwaka huu, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Barnabas Mwakalukwa alifanya ziara katika ofisi za gazeti hili na moja ya maswali aliyoulizwa yalikuwa kukamatwa kwa viongozi wa upinzani.
Akijibu swali hilo alisema, polisi wanapokwenda kuwakatama wahalifu hawaangalii vyama vyao au mambo mengine.
Maoni ya wachambuzi
Wachambuzi waliotakiwa kutoa maoni yao kuhusu hali hiyo walisema, inaweza kuwajenga zaidi wanasiasa hao huku baadhi wakipendekeza kusoma upepo wa kisiasa.
Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangalla alisema changamoto hizo zinazojitokeza kwa upinzani, unauongezea nguvu na ushawishi zaidi kwa wananchi. “Kwa hiyo ninaamini kuwabana wapinzani kwa kutumia nguvu hiyo ni kuwaongezea nguvu, mfano mzuri utakumbuka walivyojitokeza kuunga mkono upinzani kwenye uchaguzi wa 2015, licha ya vikwazo, kashfa kwa wagombea wa upinzani lakini wananchi hawakujali, kwa hiyo kila tukio wananchi wanalipima,” alisema.
Profesa huyo wa Sayansi ya Siasa na Utawala Bora alisema hofu ya matokeo ya uchaguzi mwaka 2015, ndiyo imechangia kujitokeza kwa mazingira haya baada ya CCM kufanya tathmini na utafiti wa kushuka kwa umaarufu wake katika uchaguzi huo.
Mwenyekiti wa Baraza la Katiba Zanzibar, Profesa Abdul Sherrif alisema kujijenga au kudhoofika kwa upinzani kunategemea hali ya matukio na uvumilivu huku akionyesha hofu ya kudhoofika zaidi kupitia mgogoro wa CUF.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Utawala Bora Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema kabla ya mfumo wa vyama vingi, chama tawala kilikuwa na upinzani wa ndani ya chama tu na siyo nje hivyo kiliweza kuwashughulikia wanachama wake ikiwamo kuwafukuza, huku akitolea mfano kutimuliwa kwa Maalim Seif Sharif Hamad.
“Lakini kwa mfumo wa vyama vingi, njia pekee ya kudhoofisha upinzani ni kujitangaza na kazi inayofanywa na Rais (John Magufuli), kukamata mafisadi, kuwajibisha watumishi na kurejesha nidhamu. Haya ni mambo yanayotosha kuua upinzani kwa sababu amewapokonya ajenda zao.
“Upinzani ungekuwa na wakati mgumu sana kwa utawala huu endapo angewaacha huru, wasingekuwa na ajenda yoyote ingefika wakati wangempongeza lakini kwa sasa inabidi watumie ‘Political sympathies’ kama mtaji wao kwa wananchi, wakilalamika wananchi wanawaonea huruma na inawajenga.”
Kukamatwa wabunge Chadema
Katika hatua nyingine, wanasheria kadhaa wametaka kujua sheria inayotumiwa na polisi kuwakamata wabunge wa upinzani wanaokwenda kwenye majimbo ya wenzao kwa ajili ya kujumuika nao kisiasa au maendeleo.
Wamesema hayo siku nne baada ya kukamatwa kwa Mbunge wa Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya kwa madai ya kushiriki shughuli za kisiasa nje ya jimbo lake la uchaguzi.
Bulaya alikamatwa kwa agizo la Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe kwa madai ya kutekeleza amri halali ya Serikali ya kuzuia wabunge kushiriki siasa nje ya majimbo yao ya uchaguzi.
Mbali na Bulaya, viongozi wengine wa chama hicho akiwamo katibu mkuu wake, Dk Vincent Mashinji, Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe na wa Viti Maalumu, Zubeda Sakuru pia walikamatwa na polisi.
Dk Mashinji alikamatwa na viongozi wenzake wa Chadema walikamatwa Julai 15 wakiwa wanafanya kikao cha ndani ikiwa ni ziara ya kukagua shughuli za chama Kanda ya Kusini, wilayani Nyasa Ruvuma.
Wakili na Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk James Jesse alisema matamko siyo sheria hivyo polisi wanapomkamata mtu kwa kuyafuata haieleweki wanatumia sheria ipi. Alisema ili ikamilike kuwa sheria, lazima ipelekwe bungeni na ipitishwe.
Alifafanua kuwa Rais anaruhusiwa kutoa matamko na yakawa sheria katika baadhi ya maeneo, pia zitakuwa ni sheria ndogondogo, “Hawezi kufanya hivyo kwenye masuala ya jinai,” alisema Dk Jesse.
“Hata hizo sheria ndogondogo zinazopitishwa kwa matamko pia zinaangalia zisije kukinzana na Katiba, ndiyo maana Bunge lina nafasi nzuri ya kupitisha. Kwa mfano, matamko ya kutokufanya mikutano yanakinzana na Katiba inayotoa nafasi ya uhuru wa kutoa maoni.”
Alisema kifungu cha kwanza cha Ibara ya 18 cha Katiba kuhusu haki ya uhuru na mawazo kinasomeka, “Bila kuathiri sheria ya nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake na kutafuta, kutoa na kupokea habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.”
Alisema Katiba hiyo ilitungwa mwaka 1977 na kufanyiwa marekebisho mwaka 1984 na si kupitia matamko ya mikutano.
“Ndiyo maana wengi waliokamatwa hawafunguliwi kesi kwa kufanya mikutano, lazima litafutwe jambo lingine tofauti na mkutano ili kuwapa polisi uhalali wa ukamataji huo,” alisema Dk Jesse.
Mwanasheria Charles Rwechungura alisema matamko yanayopaswa kutumiwa kama sheria ni yale yanayotolewa kulingana na nyadhifa na maeneo.
Akitoa mfano, alisema mkuu wa wilaya au mkoa anaweza kutoa tamko la kiusalama katika eneo lake, kwa kuwa ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama.
Alisema wanaokamatwa kwa kuzuiwa kufanya mikutano kwa madai ya kutekeleza tamko la Rais kisheria hawawezi kushtakiwa kwa tamko, labda kuwe na kitu kingine mbadala.
“Litatafutwa kosa la kisheria, hawawezi hata kidogo kutumia tamko kuwasimamisha mahakamani, kwa sababu matamko, siyo sheria,” alisema Rwechungura.
Wakili wa Crax Law Partners, Hamza Jabir alisema kukamatwa kwa viongozi hao kunategemea maagizo ambayo polisi wamepewa na inawawia vigumu kukataa kutokana na mazingira yao ya utendaji.
Alisema iwapo wamepewa maagizo na viongozi wa juu, kwa sheria zao hawana budi kutekeleza.
Alisema anayekamatwa na polisi siyo mfungwa, bali mtuhumiwa hivyo ana haki ya kuomba dhamana na kujitetea mahakamani ili kuthibitisha kama alionewa au la.
“... Lakini Jeshi la Polisi likipewa maelekezo ni ngumu kuyapinga,” alisema Jabir.
No comments:
Post a Comment