Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi katika mamlaka hiyo, Richard Kayombo amesema wakati wowote kuanzia leo Alhamisi, Agosti 3 watakuwa tayari wamekamilisha taarifa yote ya ukaguzi huo na kuiweka wazi kwa umma.
Kayombo ametoa kauli hiyo leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku ya mwisho tangu Rais John Magufuli alipotoa agizo la siku 14 la kufungia vituo vyote vya wafanyabiashara wa mafuta wanaokwepa kufunga EFDs katika vituo vyao.
Akiwa katika uzinduzi wa barabara ya Kigoma-Biharamulo-Lusahunga, Rais Magufuli alisema ni heri Taifa kukosa mafuta kwa muda kuliko kuvumilia wakwepa kodi.
"Tunaomba uvumilivu wa kukamilisha taarifa yote inayohusiana na ukaguzi huo, tutaeleza kila hatua zilizofanyika, tumefungia wangapi na hatua nyingine za TRA,” amesema Kayombo.
"Tunajua muda wa agizo umekamilika, lakini haipendezi kutoa taarifa nusunusu, tuko kwenye hatua za mwisho tutawaeleza (vyombo vya habari)," amesema.
Ukaguzi huo unaendelea kufanyika ikiwa ni sehemu ya kuchochea kasi ya utekekezaji wa kampeni ya TRA ya "kagua utoaji risiti na kudai risiti".
Kwa mujibu wa TRA, mteja akinaswa hana risiti atatozwa faini inayoanzia Sh300, 000 hadi Sh1.5 milioni na muuzaji asipotoa atatozwa faini inayoanzia Sh3 milioni hadi Sh4.5 milioni.
No comments:
Post a Comment