Wednesday, August 16

Rais wa Jamhuri ya Guinea Bissau ameahidi nchi yake itaridhia itifaki


Raisi wa Mahakama akitambulisha Jaji Matusse kwa Raisi was Guinea Bissau Ikulu. Kushoto wa pili ni Makamu wa Raisi wa Mahakama Jaji Ben Kioko.

 Rais wa Jamhuri ya Guinea Bissau Mheshimiwa Jose Mario Vaz ameahidi kuwa, nchi yake itaridhia itifaki iliyoanzisha mahakama ya Afrika ya haki za  binadamu na watu (AfCHPR) mapema iwezekanavyo .

Akizungumza na ujumbe wa mahakama hiyo ulioko katika ziara ya kikazi nchini Guinea Bissau, Rais Vaz alisema hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba Guinea Bissau ilikuwa miongoni mwa nchi za mwanzo za umoja wa Afrika kutia saini itifaki iliyoanzisha AfCHPR mwaka 1998.

Katika mazungumzo yake na ujumbe huo ulioongozwa na rais wa AfCHPR mheshimiwa Jaji Sylvain Ore kiongozi huyo wa Guinea Bissau alielezea kuridhishwa kwake na madhumuni ya kuanzishwa kwa mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu na kuongeza kuwa masuala ya haki za binadamu yana umuhimu mkubwa katika kufikiwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika nchi za Afrika na kuwaondoa wananchi wake katika lindi la umaskini na ufukara.

“Ahadi yangu ni kuhakikisha kuwepo kwa haki za binadamu katika nchi yangu” alisisitiza Rais Vaz.

Ujumbe wa AfCHPR pia ulikutana na waziri mkuu wa Guinea Bissau Mheshimiwa Umario Sissoco Embalo ambaye alisema mamlaka husika za nchi yake zitaandaa nyaraka zinazohitajika ili kuzipeleka katika bunge la taifa nchini humo kwa lengo la kuridhia itifaki iliyoanzisha mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu.

“Mimi ni muumini mkubwa wa umajumui wa Afrika (Pan-Africanism) na nitafanya kila linalowezekana kuimarisha taasisi za umoja wa afrika” alisisitiza waziri mkuu huyo.

Rais wa AfCHPR jaji Ore na ujumbe wake ambao umejumuisha Makamu wa rais wa mahakama hiyo Mheshimiwa Jaji Ben Kioko, Mheshimwa Jaji Angelo Matusse na baadhi ya maafisa wa ofisi ya msajili wa AfCHPR pia ulikutana na Jaji Mkuu, waziri wa masuala ya jamii na pia kamisheni ya haki za binadamu ya Guinea Bissau.

Jaji Ore alisema ilikufanikisha malengo ya mahakama na pia kuimarisha mfumo wa haki za binadamu barani Afrika nchi nyingi za umoja wa afrika hazina budi kuridhia itifaki iliyounda AfCHPR kwa mujibu wa kifungu cha 34(6) na kutoa tako rasmi la kutambua na kukubali a mamlaka ya mahakama kuweza kupokea kesi za watu binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs)

Hadi sasa ni Nchi 30 tu kati ya nchi 55 wanachama wa AU ndio zimeridhia itifaki husika.

AfCHPR yenye makao yake makuu jijini Arusha iko nchini Guinea Bissau kwa ziara ya kikazi ya siku 2 ili kukutana na viongozi na wadau mbalimbali kwa lengo la kuitangaza mahakama hiyo.

No comments:

Post a Comment