Tuesday, August 29

Polisi aeleza alivyohangaika na Masogange

Masogange (kushoto) akiondoka katika Mahakama

Masogange (kushoto) akiondoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana baada ya kesi yake kuahirishwa. Picha na Omar Fungo 
Dar es Salaam. Mahakama ya Kisutu imepokea ripoti ya uchunguzi wa sampuli ya mkojo ya Msanii Agnes Gerald maarufu kama Masogange, kutoka ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali kama kielelezo.
Kielelezo hicho kiliwasilishwa na Mkemia Elias Mulima baada ya kutolewa uamuzi na Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Hatua hiyo inafuatia baada ya mawakili wa Masogange, Nehemia Nkoko na Ruben Simwanza kupinga mahakama isipokee ripoti hiyo kama kielelezo.
Ripoti hiyo ilitolewa na mkemia huyo ambaye alipima sampuli hiyo ya mkojo, ili kuthibitisha kama una dawa za kulevya au la.
Baada ya kupokelewa kwa ripoti hiyo ya uchunguzi. Wakili Simwanza alimuuliza awali shahidi huyo kuwa ana uhakika huo mkojo ni wa Masogange. Mulima akajibu kuwa ana uhakika sampuli ya mkojo aliyoifanyia uchunguzi ilikuwa ni ya Agnes.
Kwa upande wa shahidi mwingine wa mashtaka ambaye ni Ofisa wa Polisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum, WP Judith alieleza namna alivyokabidhiwa Masogange, alivyompeleka kwa mkemia na alivyotoa sampuli ya mkojo.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Constantine Kakula, Judith alidai siku ya tukio ndiye aliyempeleka Masogange chooni kutoa sampuli ya mkojo.
Alidai kuwa siku hiyo alimpeleka hadi chooni Masogange, kutoa sampuli ya mkojo na mshtakiwa aliingia chooni yeye alibaki nje na kwamba baada ya kutoka na sampuli ya mkojo, aliichukua na alikwenda kumkabidhi Koplo Sospeter.
Shahidi huyo, alimtambua Masogange mahakamani hapo kwamba ndiye aliyekabidhiwa na kiongozi wake Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu, Ramadhan Kingai kumpeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kufanyiwa uchunguzi.
Alidai alimpeleka Februari 15 kutokana na tuhuma za kutumia dawa za kulevya au kusafirisha. Alidai aliambatana na Koplo Sospeter hadi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na walifika saa saba mchana.
Aliendelea kusai kuwa akiwa mapokezi alikabidhiwa chupa ndogo ya plastiki iliyokuwa na namba ya maabara 006/2017, alielekezwa ampeleke kwenye choo maalumu kwa ajili ya kutoa sampuli ya mkojo.
Shahidi huyo alidai kuwa aliondoka na mshtakiwa hadi chooni, alitoa sampuli ambayo aliichukua na kumkabidhi Koplo Sospeter.
Sehemu ya mahojiano ya Wakili Semwanza anayemtetea Masaogange na shahidi huyo yalikuwa hivi;-
Wakili: Mshtakiwa kwa mkemia alitoa mkojo wa rangi gani?
Shahidi: Ulikuwa na rangi ya njano iliyopauka.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa Alhamisi hii kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

No comments:

Post a Comment