Tuesday, August 29

Bulaya aruhusiwa, kufanyiwa upasuaji nyama za pua

Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya akiwa

Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya akiwa ameshika Bibilia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wakati akisubiri kupewa dawa baada ya kuruhusiwa kurudi nyumbani jana. Mbunge huyo alilazwa kwa wiki moja akitibiwa ugonjwa wa pumu. Picha na Herieth Makwetta 
Dar es Salaam. Mbunge wa Bunda (Chadema), Ester Bulaya, ambaye ameruhusiwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa, atafanyiwa upasuaji.
Bulaya, ambaye alipata tatizo la kupumua baada ya kuzidiwa akiwa mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi Tarime, alilazwa kwa siku nane tangu alipofikishwa hospitalini wilayani Tarime mwanzoni mwa wiki jana na kuhamishiwa Muhimbili ambako alilazwa Sewahaji wodi namba 18.
Akizungumza na gazeti hili jana, Halima Mdee, mbunge wa Kawe(Chadema) na ambaye amekuwa akishughulikia matibabu ya mbunge huyo tangu alipolazwa, alisema madaktari wamemruhusu kutokana na hali ya afya yake kutengemaa, lakini wamempa masharti.
“Ameruhusiwa, anaweza akatoka leo (jana). Matibabu ya awali ilikuwa ni ile pumu na yamekamilika kwa kiasi kikubwa, lakini pia kuna dozi ataendelea nayo. Siku kadhaa zijazo atatakiwa aripoti kliniki,” alisema Mdee.
Alisema baada ya kipimo cha CT Scan ambacho madaktari walitumia kuhakikisha kama ana maambukizi yoyote puani au nyama za pua ambazo pia husababisha mtu akose hewa na hatimaye kuchangia kupata matatizo hayo, wamegundua kwamba kuna nyama za pua ambazo atafanyiwa upasuaji kuzirekebisha.
“Tunachokisubiri ni huo upasuaji mdogo kwa ajili ya kupunguza nyama. Tatizo lake la pumu limeangaliwa na anaendelea vizuri,” alisema Mdee.
“Kwa maelekezo aliyopewa na madaktari atafuata na tatizo hilo haliwezi likatokea tena baadaye.”
Bulaya azungumza
Akizungumza mara baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, Bulaya alisema kwa sasa anaendelea vizuri na ameambiwa apumzike kwa siku kumi na ametakiwa kuhudhuria kliniki kila wiki kwa ajili ya kuangaliwa afya yake.
Akiwa mwanasiasa, Bulaya hakukosa neno la kuwaambia wapigakura wake kuhusu hali yake.
“Kikubwa tu nawaambia niko vizuri wasiwe na wasiwasi, afya yangu inaimarika,” alisema mbunge huyo kijana.
“Nikishakuwa sawa nitakwenda kuungana nao kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Kwa sasa najitahidi kusimama mwenyewe, nakula na kujihudumia mwenyewe. Kikubwa waniombee kwa Mungu.”
Akielezea chanzo cha tatizo lake, Bulaya alisema kwa muda mrefu amekuwa na tatizo la pumu, lakini anapokaa kwenye mazingira yasiyo rafiki hubanwa zaidi na ugonjwa huo unaoathiri mfumo wa kupumua.
“Ilinitokea nikiwa mahabusu. (Nadhani) ilichangiwa na ule msongamano wa watu, hewa ilikuwa ndogo,” alisema Bulaya.
“Nadhani ile kunikimbiza kwenye vumbi sana wakati nimetokea Tarime, kunipeleka chumba cha mahabusu. Tulipita barabara yenye vumbi jingi. Nakumbuka nilisikia kubanwa na pumzi na baadaye niliishiwa nguvu.”
Bulaya alikamatwa Agosti 18 kwa madai ya kuingia jimbo la Tarime Vijijini ambako alihudhuria mkutano wa hadhara na kutoa mifuko 50 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Nyamongo.

No comments:

Post a Comment