Wednesday, August 23

Kikwete ajipanga kuanzisha kiwanda


Rais wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete (kulia)

Rais wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete (kulia) akiangalia mahindi ya njano yanayoendelea kuvunwa shambani kwake Msoga,  Chalinze mkoani Pwani. Kikwete amesema ataitumia nafaka hiyo kwa virutubisho na malisho ya ng’ombe wake anaowafuga kijijini hapo. Picha na Julieth Ngarabali 
Chalinze. Rais wa Awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema yupo mbioni kufungua kiwanda cha usindikaji wa maziwa na siagi kwa sababu sasa anapata lita zaidi ya  200  za maziwa kila siku.
Akizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake Msoga jana, Kikwete alisema mpango alionao ni kuanzisha kiwanda cha kusindika maziwa na siagi kwa sababu ana uhakika atakimudu.
Alisema anaweza kufungua kiwanda hicho kwa sababu kwa sasa ana ng’ombe zaidi ya 400 na  mpango wake ni kuongeza wengine wa maziwa.
“Inawezekana kabisa kwa sababu ukitaka kufungua kiwanda kama hicho unatakiwa kuhakikisha kwamba una ng’ombe wa kutosha, malisho  na  uhakika wa kuwapatia matibabu,’’ alisema
“Nimeanza kilimo na ufugaji  tangu  miaka ya 1988/1989 na ndiyo maana namudu kusimamia na kupata faida,” alisema  Kikwete.
Alisema watu wasipende kusubiri  muda wa kustaafu ndiyo waanze kujishughulisha na kilimo au ufugaji kwani kazi hizo zina changamoto zake ambazo kama mtu hakuzizoea tangu awali anaweza kukwama.
Alisema msimu huu amelima ekari 30 za mahindi ya njano na jana  alivuna ekari nne tu za kwanza.
Mstaafu huyo alifafanua kuwa aliamua kulima aina hiyo ya mahindi ili aweze kupata malisho na virutubisho vya mifugo yake kwani nafaka hizo zina nguvu zaidi ya mahindi ya kawaida.
Alipoulizwa kuhusu hali ya kisiasa hapa nchini na uchaguzi mkuu wa Kenya, Kikwete alisema ‘no comment’ (sina cha kusema) kwani yeye ni mkulima na mfugaji na mambo mengine alishawaachia wengine.
Alisema kuwa hata akiwa nyumbani kwake ametulia hapendi kuzungumzia ya wengine waliopo sasa kwani kila nyakati na watu wake na staili yake.
“Jamani mimi niulizeni mambo ya kilimo na ufugaji tu, masuala mengine sijui ya nchi au hata hili la uchaguzi wa Kenya msiniulize jamani, mimi kwa sasa ni mstaafu, mambo ya serikali wapo wenyewe, mimi nilishamaliza kazi yangu, kama kushauri au kufanya nilishafanya niliyoweza na nikawaachia wengine,”alisema Kikwete ambaye aliongoza nchi kwa vipindi viwili vya miaka kumi kuanzia mwaka 2005 mpaka 2015 .

No comments:

Post a Comment