Kamanda Muslimu alitoa kauli hiyo leo asubuhi jijini Mbeya wakati akitoa pongezi kwa Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mwambelo kwa kazi nzuri aliyoifanya kusimamia na kuchukua hatua kali kwa madereva na sasa vivuko hivyo vimekuwa vikiheshimiwa.
Amesema Mbeya ndio mkoa pekee ambao madereva wa vyombo vya moto wamekuwa na utii wa hali ya juu maeneo ya vivuko vya watembea kwa miguu kusimama takribani sekunde 45 hata kama hakuna anayevuka muda huo jambo linalopaswa kuigwa na watu wote nchini.
“Nimefurahishwa sana na madereva wa Mbeya namna ambavyo wanaheshimu zebra, na hii imetokana na usimamizi mzuri wa mkuu wa usalama barabarani mkoani Mbeya. Pongezi nyingi kwako, na hii nataka iwe mfano kwa wakuu wote wa usalama barabarani nchini,”alisema Kamanda Muslimu.
Alisema lengo lake ni kuona wanaondoa askari wote barabarani, wakapangiwe kazi nyingine na madereva wajiongeze wenyewe huku akisisitiza kwamba dereva akikamatwa kwa kosa la kutoheshimu zebra atapigwa faini na kupelekwa moja kwa moja mahakamani.
Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mbeya, Butusyo Mwambelo alimweleza Kamanda Muslimu kwamba njia aliyoitumia kuhakikisha madereva wanaheshimu alama za barabarani hakutaka kuwatuma askari wake muda wote kusimamia zoezi hilo bali alikwenda mwenyewe kusimama sehemu za zebra na kuwakamata madereva wote wasioheshimu alama za vivuko vya watembea kwa miguu, kuwalipisha faini na kuwapeleka mahakamani.
‘Nilipanga siku tatu tatu kwa kila eneo la alama za zebra nilisimama pale kutoa elimu kwa madereva lakini pia niliwakamata wasiotaka kuheshimu zebra niliwapiga faini na kuwapaleka mahakamani.’
Kamanda Butusyo amesema kwa sasa madereva wameelewa na wamekuwa na utii wa hali ya juu kwenye alama za vivuko vya watembea kwa miguu kutokana na hatua kali zinazochukuliwa dhidi yao.
Balozi na mdau wa usalama barabarani jijini Mbeya, Wiseman Luvanda alisema kitendo cha madereva kuheshimu vivuko vya watembea kwa miguu kimesaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza ajali ndani ya jiji hilo kwani madereva wamekuwa wakitembea mwendo usio hatarishi.
No comments:
Post a Comment