Siku Rais John Magufuli alipotangaza kufuta shamrashamra za Sherehe ya Uhuru, Desemba 2015 na kuamuru Sh4 billioni zilizotengwa kugharamia siku hiyo zielekezwe katika mradi huo, watumiaji wa mara kwa mara wa barabara hiyo walianza kufikiria ahueni watakayopata kutokana na kero ya foleni iliyodumu kwa miaka kadhaa. Huo ni upande mmoja wa yanayohusu barabara hiyo.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa furaha ya kukamilika kwa bararaba hiyo imekuja na machungu yanayotokana na ongezeko kubwa la ajali zinazokatisha maisha ya watu na kuwaacha wengine wengi na vilema vya maisha.
Kuna sababu kuu mbili zinazokusukwa na jambo hili; kwanza, vizuizi vya zenge viliyowekwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) maeneo kadhaa ya barabara hiyo vinasababisha ajali hasa nyakati za usiku, ama kwa kuwa na viakisi mwanga dhaifu au kutokuwapo kabisa.
Pili, watembea kwa miguu wamekuwa wakijikuta kwenye wakati mgumu kuvuka kutoka upande mmoja hadi mwingine wa njia hizo tatu, ambapo watu wanapoteza maisha na kupata ulemavu baada ya kugongwa wakivuka barabara.
Vizuizi vya zege
Baada ya kukamilika upanuzi wa barabara hiyo, vizuizi vya zege viliwekwa katika maeneo tofauti vikitumika kuzuia magari yanayotoka katika njia ndogo na kuingia barabara kuu. Mfano huo ni halisi katika eneo la Sayansi, ambapo vimewekwa kuzuia magari yanayotoka Kijitonyama na Sinza yasikatize na kuingia barabara kuu.
Vizuizi hivyo vimesababisha ajali mbaya za magari katika maeneo ya Makumbusho, Sayansi, Bamaga na Victoria hasa wakati wa usiku.
Baadhi ya maeneo kama vile Makumbusho mbele ya jengo la Millenium Tower na lile la kampuni ya Tigo, vizuizi hivyo vimepangwa katikati ya barabara kutumika kama eneo la usalama kwa wavuka barabara kabla ya kumalizia kuvuka. Hata hivyo, haisaidii kupunguza ajali kwa kuwa watu wengi hawajui hivyo. “Hapa tunashuhudia ajali karibu kila siku, lakini ajali nyingi zinatokea kuanzia siku ya Alhamisi na nyakati za usiku kwa sababu zege hizo hazina reflectors (viakisi mwanga). Hivi tunavyoongea jana tu ajali mbaya ilitokea kwa bahati hakuna aliyeumia,” anasema dereva wa bodaboda katika kituo cha Sayansi, Alexander Kione.
“Hizi reflector zimepauka na ikifika nyakati za usiku hazionekani, hivyo inakuwa ni ngumu kwa dereva asiyeifahamu vizuri hii barabara kujua kama mbele kuna nini,” aliongeza.
Mapema wiki hii, mtu aliyefahamika kwa jina la Msiba Joseph alipata ajali katika eneo la Sayansi baada ya kugonga vizuizi hivyo saa saba usiku.
Mwandishi alishuhudia gari lake likiwa limeharibika vibaya, ingawa hakupata majeraha makubwa baada ya kusaidiwa na mfuko wa hewa unaotoka kwenye usukani kumuepusha na madhara ambayo angepata.
“Ninakwambia kesho haya huyakuti..kesho huyakuti. Sisi ndio tunaosimamia hii barabara na sasa yanataka kuua. Mungu ni mwema sana ndugu zangu. Mungu ni mwema,” alisisikika akisema muda mfupi baada ya kunusurika.
Dereva mwingine wa bajaj katika eneo la Makumbusho, Kudaga Jackson alisema: “(Vizuizi) vimesaidia wanaotaka kuvuka barabara lakini ni tatizo kubwa kwa wanatumiaji wa vyombo vya moto hasa wakati wa usiku.”
Meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama alisema kuwa kwa upande mmoja yapo mambo ya msingi katika barabara hiyo hayajakamilika, huku upande mwingine akiwalaumu madereva wasio makini kusababisha ajali hizo.
“Kusema kweli upanuzi haukufikia mwisho. Kuna mambo kweli hayajafanyika lakini hivi vizuizi vya zege tuliviweka kwenye middle lane (njia ya katikati) ambayo haikupaswa kutumika. Ajali nyingi zinatokea usiku mnene. Hizo gari zinazotembea usiku na kuchukua lane (njia) ni kubwa kiasi gani?” alihoji Ndyamukama na kuongeza:
“Kuna wakati tulitaka kuviondoa (vizuizi) eneo la Sayansi lakini tulibishana sana na polisi waliotaka viendelee kuwepo kuwazuia madereva wanaotoka upande wa Sayansi na Sinza ambao husababisha msongamano. Sasa tuna mpango wa kuyaondoa iwe huru kwa wote tu, halafu tuone itakuwaje.”
Alama za pundamilia
Ujenzi wa barabara hiyo pia haukuzingatia mahitaji ya watembea kwa miguu kwa kutoweka mazingira rafiki na salama kwa wavukaji.
Watembea kwa miguu hujikuta katika wakati mgumu inapofika wakati wa kukatiza njia hizo tatu kwa kuwa hakuna mahali salama pa kusimama pale mtu anaposubiri gari za upande wa pili zipite ili avuke. “Utakuta mtu amesimama katikati ya barabara kupisha magari lakini ghafla linakuja gari katika mwendo mkali kwa kutumia barabara aliyosimama na kumgonga,” alisema dereva wa bajaj, Yohana Silvanus.
Mtembea kwa miguu, Anna Richard alisema: “Watu wengi wanagongwa katika alama hizi za pundamilia. Kwa kweli ni ngumu sana kusimama katikati ya barabara kupisha magari kwa sababu hata tunaposimama sio sehemu sahihi maana magari yanapita pia.”
Polisi wanasemaje?
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Kinondoni, Solomoni Wangamila alisema pamoja na upungufu katika kuweka vizuizi hivyo, watumiaji wa barabara pia wanapaswa kulaumiwa zinapotokea ajali. “Tatizo yale mawe ya zege yamewekwa katika maeneo ambayo yako katikati ya barabara. Hili si jambo kubwa sana, lakini tatizo ni kwamba watu wanayagonga kutokana na mwendokasi na ulevi,” alisema kamanda huyo.
“Watumiaji wengi wa barabara ni watu wasiofuata sheria kwa hiari mpaka waone askari amesimama pembeni, ndiyo maana ajali nyingi katika eneo hilo zimekuwa zikitokea nyakati za usiku wakati madereva wakiwa wamelewa.”
Alikataa madai kuwa ajali katika eneo hilo hutokea mara kwa mara, huku akikiri kuwa uharibifu wa mali za watumiaji umekuwa mkubwa.
Askari wa usalama barabarani katika Kituo cha Polisi Oysterbay aliyeomba jina lake lihifadhiwe alitoa maoni tofauti akisema, “nakueleza haya mawe ya zege yamechukua maisha ya watu wengi sana. Kila siku watembea kwa miguu wanagongwa na usiku hawachelewi kutuita. Sisi siyo kazi yetu kuyaondoa.”
No comments:
Post a Comment