Naibu Waziri wa Nishati na Madini,Dk Medard Kalemani
Dk Kalemani hayo leo mara baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa vituo vya kupoozea umeme vya Kurasini na Kigamboni.
“Kama maagizo haya hayatafuatwa ama niondoke mimi au uondoke wewe na watendaji wengine, kama mtashindwa kutekeleza mnieleze hapa hapa,”amesema huku watendaji hao ambao waliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Tito Mwinuka wakikaa kimya kuashiria kuwa watatekeleza.
Katika agizo la kwanza, Kalemani alisema kuna wakazi 350 wa Kigamboni ambao walishailipa Tanesco ili waunganishiwe umeme lakini wamekaa muda mrefu bila kupata huduma hiyo.
Amesema hadi Agosti 30, mwaka huu wateja hao wawe wameunganishiwa umeme vinginevyo wasubiri atachukua hatua.
“Nawaambia tafuteni vifaa kama nguzo za umeme popote zilipo lakini nataka wafungiwe kama nilivyoagiza kwa kuwa nimechoka na malalamiko yao,”alisema.
Dk Kalemani ametembelea eneo la Kigamboni Kimbiji ambako Tanesco walinunua eneo kwa ajili ya kujenga kituo cha kupoozea umeme.
Awali Meneja wa Tanesco wa Mkoa wa Temeke, Jahulula Jahulula alimweleza waziri kuwa kituo hicho kitaanza kujengwa mwaka ujao na kukamilika mwaka 2019.
Kalemani alishangazwa ujenzi wa kituo hicho kuchukua muda mrefu hivyo akaagiza kuwa ujenzi uanze baada ya miezi mitatu na ukamilike Machi 2018.
“Nilipotembelea hapa mwanzoni mwa mwaka huu nilikuta eneo hili mkanieleze kuwa mtajenga sub station, leo tena nakuja hapa mnanihadithia yaleyale hamjafanya chochote,”amesema.
“Vituo hivi vikijengwa vitasaidia kuondoa matatizo ya umeme ambayo wananchi wanatulalamikia kila siku,”amesema.
Amesema aliwaelekeza wajenge uzio kwenye eneo hilo la kiwanja hicho lakini wameshindwa kutekeleza agizo lake.
Katika agizo la tatu, Kalemani alisema ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme cha Kurasini ukamilike Septemba 15 mwaka huu.
Amesema kituo hicho kimechukua muda mrefu kujengwa lakini ameona hatua waliyofikia imemridhisha.
“Nimeridhika na hatua mliyofikia hivi sasa lakini nataka muongeze bidii na kikamilike Septemba 15, nimechoka Mbagala wanalia kila siku kwa sababu umeme unakatika mara kwa mara,”amesema.
Kwa upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco,Dk Mwinuka alisema maagizo yaliyotolewa na Naibu Waziri watayatekeleza.
“Tutaongeza speed (kasi) ya kufanya kazi ili kutekeleza maagizo ya waziri ili kuondoa ukosefu wa umeme unaowakabili baadhi ya wananchi,” amesema.
Hata hivyo,hakusema kwa nini ujenzi wa kituo hicho haujaanza licha ya kiasi cha Sh5 bilioni kutengwa kwa ajili ya kazi hiyo
No comments:
Post a Comment