Thursday, August 24

Haya ndiyo maswali 22 ya DC Hai kwa walimu



Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa 
Moshi. Wakati sakata la Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa kumsweka mahabusu mwalimu wa sekondari kwa kushindwa kutaja jina lake likiendelea kuzua mjadala, imedaiwa kuwa siku hiyo aliwauliza walimu aliokuwa na kikao nao maswali 22.
Tukio hilo la Byakanwa kudaiwa kuamuru kukamatwa na kuwekwa mahabusu mwalimu huo wa Shule ya Sekondari Lerai, Erasto Mhagama, ndilo limekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii.
Mbali na kubamba mitandao ya kijamii, walimu katika mijumuiko mbalimbali na kupitia Chama cha Walimu Tanzania (CWT) na makundi ya WhatsApp ya walimu, tukio hilo ndilo linalojadiliwa zaidi katika mitandao hiyo.
Inadaiwa baada ya mwalimu huyo kushindwa kuandika jina la mkuu wa wilaya, kiongozi huyo alimtaka achague mojawapo ya adhabu kati ya kupiga pushup au kwenda mahabusu ya polisi.
Mwalimu huyo alimweleza mkuu huyo wa wilaya kuwa asingeweza kupiga pushup kwa kuwa ana matatizo ya kiafya, ndipo mkuu wa wilaya alipoita polisi na kumpeleka mahabusu.
Hata hivyo, Byakanwa alikaririwa na gazeti hili akisema hakuamuru kuwekwa mahabusu kwa mwalimu huyo kwa sababu ya kushindwa kutaja jina lake, bali kwa makosa ya utovu wa nidhamu. Lakini mkanda wa sauti ambao ulirekodiwa kwa kutumia simu ya mkononi siku hiyo ambao gazeti hili umeusikia unamkariri kiongozi huyo akiwauliza walimu hao maswali 22.
Hata hivyo, Byakanwa alipoulizwa jana kuhusu kuwauliza walimu maswali hayo, hakukanusha wala kuthibitisha akitaka wanahabari wajiridhishe kama sauti ni ya kwake.
“Nyinyi kama vyombo vya habari mjiridhishe kama sauti ni ya DC maana mimi sijampa mwandishi yoyote sauti iliyorekodiwa ya hiyo siku,” alisema.
Byakanwa aliwataka waandishi wa habari wavute subira kwani atazungumzia tukio hilo na mengine yaliyojitokeza katika ziara yake atakapomaliza kutembelea shule zote za wilaya yake.
Ilielezwa kuwa katika kikao hicho na walimu wa shule mbili za sekondari Boma na Lerai, mkuu huyo wa wilaya alianza kwa kugawa karatasi na kuwauliza walimu kama kuna anayemfahamu.
Alipowauliza swali hilo walimu wa Shule ya Lerai, ni mmoja tu aliyesema anamfahamu ndipo alipowataka wengine wote kuandika jina lake kwenye karatasi.
Baadaye alimsimamisha mwalimu mmoja baada ya mwingine akitaka waende ubaoni kuandika maneno au kuweka majibu ya maswali atakayowauliza na maswali hayo yalikuwa kama ifuatayo:
Maswali 22
1.Nani ambaye ananifahamu?
2. Kila mmoja aaandike jina langu kwenye hiyo karatasi
3. Waziri mkuu wa awamu ya tatu ni nani?
4. Nitajie kirefu cha CDF (Chief of Defence Forces)
5. Nitajie Waziri wa Nishati na Madini
6. Andika kirefu cha DC (District Commissioner)
7. Andika neno IGP na kirefu chake
8. Andika neno CDF na kirefu chake
9. Andika CUF na kirefu chake
10. Andika CAF na kirefu chake
11. Andika neno Tanu na kirefu chake.
12. Andika TLP na kirefu chake
13. Agronomy means what?
14. Nani ni viongozi wakuu wa CUF. Baada ya kujibiwa ni Profesa Ibrahim Lipumba na Maalim Seif Sharifu Hamad akauliza mkutano wao mkuu wa mwisho ulikuwa lini?
15. Nani ni kiongozi wa CAF (Confederation of African Football)
16. Nitajie IGP (Inspekta Jenerali wa Polisi) ni nani na CDF (mkuu wa majeshi) ni nani kwa majina
17. Mwenye cheo cha CDF ni nani
18. Mwamunyange mnamfahamu? Ni Nani
19. Baada ya kustaafu Mwamunyange akaja nani?
20. Mkuu wa Majeshi kwa Kiingereza anaitwaje?
21. Rais wa CAF ni nani?
22. Andika pale ubaoni Chief of Defence Forces







No comments:

Post a Comment